Habari
Karibu katika uendelezo wa somo letu la kutafuta hazina ya maisha, tukiongozwa na kitabu cha “the alchemist “kilichoandikwa na Paulo Coelho.
Wakati Santiago na alchemist wanaendelea na safari, walikamatwa na moja ya makundi ya wapiganaji, na wakawatuhumu kwamba ni wapelelezi, ambao wametumwa na maadui na hivyo wanapaswa kuuawa.
Alchemist aliwaambia wapiganaji wale kwamba wao siyo wapelelezi, bali ni wasafiri kuelekea mapiramidi na kijana aliyenaye anaweza kufanya miujiza. Aliwaambia anaweza kujigeuza kuwa kimbunga ambacho kinaweza kufunika eneo zima. Kiongozi aliposikia hivyo, akasema ajigeuze kuwa kimbunga la sivyo atawaua. Alchemist akaomba wapewe siku tatu.
Baada ya Kuachana na wapiganaji wale, Santiago alimwangalia alchemist kwa mshangao, akamuuliza kwa nini umewaambia naweza kufanya miujiza wakati siwezi? Alchemist akamjibu hilo ndilo unalopaswa kufanya sasa, la sivyo watatuua. Santiago akamuuliza, sasa nitawezaje kujigeuza kuwa kimbunga? Alchemist akamwambia hajui, aulize dunia na asikilize lugha ya dunia.
Basi kwa siku mbili Santiago alikaa eneo la mlima na kuweza kuangalia na kuisikiliza dunia, aliangalia kila kitu kwa undani wake, akaanza kupata nguvu kulielewa jua, kulielewa upepo na vitu zingine.
Siku ya tatu wapiganaji wale waliwaita ili waje kuonesha miujiza, Santiago aliwaambia wakae eneo la chini na yeye aende kwenye kilima, kisha akaanza kuongea na dunia, jua, upepo alipeleka mawazo yake yote kwenye dunia na ghafla upepo mkali ulianza kumzunguka na kimbunga kuanza kujikusanya.
Kilikuwa kimbunga kikubwa ambacho kilifunika kabisa eneo lile, mpaka baadhi ya wapiganaji walipatwa na hofu. Kimbunga kiliendelea kuwa kikali na hawakumwaona tena Santiago, kimbunga kilipokuja kutulia wakimkuta amekaa eneo la tofauti kabisa na pale alipo kwa awali.
Miujiza huo uliwafanya waruhusiwe Kuendelea na safari yao. Kuna wakati utakutana na ugumu ambao wewe peke yako hauwezi kuutatua, katika nyakati kama hizi, kinachoweza kukuogoa ni miujiza, ambao unapaswa kuutengeneza wewe mwenyewe.
Kila mmoja wetu ana nguvu ya kutengeneza miujiza kama ataisikiliza dunia na kutumia vizuri nguvu ya akili yako. Popote unapokwama tengeneza miujiza wa kukutoa hapo.
Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio na maisha, anayejifunza kazi ya uandishi kupitia kwa waandishi wengine.
Maureen Kemei
Blog
kufikirichanya.wordpress.com