Habari
Karibu sana katika uendelezo wa somo letu la kutafuta hazina ya maisha. Tukiongozwa na kitabu cha ‘the alchemist’ kilichoandikwa na Paulo Coelho.
Santiago alifika chini ya mapiramidi na kuanza kuchimba akitafuta hazina yake, wakati anaendelea kuchimba walikuja watu ambao walimnyang’anya dhahabu aliyokuwa nayo na kumpiga vibaya.
Baada ya kugundua hakuna kitu kingine cha thamani wanachoweza kuchukua, waliamua kumwacha na kuondoka. Lakini mmoja alimuuliza anafanya nini pale, akamjibu anatafuta hazina yake ambayo aliona kwenye ndoto.
Mtu huyo alicheka sana, akamwambia na wewe unaamini huo ujinga? Akamwambia ata yeye alipata ndoto kama hiyo kwamba hazina yake ipo kwenye kanisa lililopo Uhispania, lakini hajajisumbua nayo.
Baada ya kusikia hivyo, Santiago ndiyo alielewa safari nzima, kumbe hazina yake ilikuwa pale alipoipata ndoto yake. Hivyo alirudi kwenye like kanisa, akachimba na kuikuta hazina. Lakini kilichomnufaisha siyo hazina aliyopata, bali safari nzima ya kutafuta hazina hiyo.
Hii ndiyo funzo kuu la hadithi hii, funzo ambalo ukilielewa maisha yako yatakuwa na maana kubwa.Watu wengi wamekuwa wakipata maono, ndoto au kuweka malengo wakiamini kwamba watakapofikia ndiyo watakuwa na furaha. Furaha haipo kwenye kufikia ndoto, maono au malengo, bali ipo kwenye safari nzima ya kufikia ndoto hiyo.
Hazina yako ipo hapo ulipo sasa, unatembea nayo, hazina yako ni safari unayopita kila siku, ni jinsi unavyovuka vikwazo vya kila aina. Usisubiri mpaka mwisho ndiyo ufurahie, bali furahia kwa kila hatua unayopita.
Mwisho kabisa unapokuwa na ndoto au maono au lengo, ukipambana kuyafikia, usipumzike na kuona umeshashinda, badala yake weka ndoto, maono au lengo jingine. Yaani hakikisha kila siku ya maisha yako Kuna kitu kikubwa unachokifanyia kazi, na hapo maisha yako yatakuwa na maana wakati wote.
Kila siku hakikisha Unapiga hatua kuelekea kwenye hazina ya maisha yako, ambayo unayo hapo ulipo sasa.
Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio na maisha, pia anajifunza kazi ya uandishi kupitia kwa waandishi wengine.
Maureen Kemei
Blog kufikirichanya.wordpress.com
Email
kemeimaureen32@gmail.com