Habari
Nikukaribishe sana rafiki tujifunze tabia hizi zinazoweza kutufikisha kwenye mafanikio makubwa, tukilielewa vizuri na kuchukua hatua.
Kwenye kitabu cha high performance habits (how extraordinary people become that way). Brandon Burchard anatushirikisha tabia sita zitakazotuwezesha kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yetu.
Brandon anatushirikisha tabia hizi kutokana na uzoefu wake binafsi, baada ya kuwakochi watu wenye mafanikio makubwa. Lakini pia ameingia kwenye tafiti nyingi za kisayansi na kijamii na kuweza kuona mchango wa tabia hizo kwenye mafanikio.
Kupitia uzoefu huo binafsi na matokeo ya tafiti, Brandon anatudhibitishia kwamba tukiweza kuziishi tabia hizi sita, tutaweza kuwa na mafanikio makubwa sana.
Brandon anatushirikisha tabia hizo sita na hatua tatu za kuchukua kwenye kila hatua hili ziweze kuwa na manufaa kwenye maisha yetu.
Tabia hizi sita amezigawa kwenye makundi mawili, kundi la kwanza ni tabia binafsi na kundi la pili ni tabia za kijamii.
TABIA BINAFSI.
Kundi la kwanza la tabia za kimafanikio ni tabia binafsi, ambazo zinamhusisha mtu pekee.
Zifuatazo ni tabia tatu zilizoko kwenye kundi hili.
TABIA YA KWANZA. TAFUTA UWAZI.
Tabia muhimu sana kwenye maisha yetu ni kutafuta uwazi, tu natafuta uwazi kwa kujijua wenyewe, yaani misingi unayoisimamia, uimara wako na hata madhaifu yako.
Pia unakuwa na uwazi pale unajua nini hasa unataka kwenye maisha yako, maono yako makubwa pamoja na malengo uliyonayo.
Lakini pia uwazi inahusisha kujua jinsi ambavyo utafikia maono na malengo yako, yaani mipango unayofanyia kazi ili kufika kule unakotaka kufika.
Kama hujijui wewe mwenyewe, hujui unakokwenda na hujui unafikaje, haijalishi unachukua hatua kubwa kiasi gani, huwezi kufikia mafanikio makubwa.
HATUA TATU ZA KUCHUKUA KWENYE TABIA YA KWANZA.
Moja. Tengeneza maono yako kwenye maeneo manne muhimu ya maisha yako.
Eneo la kwanza ni maisha binafsi, hapa unapaswa kuwa na maono yako binafsi, unataka kuwa nani, jione kama tayari umeshafika kule unakotaka kufika na endesha maisha yako kama tayari umeshafanikiwa.
Eneo la pili ni maisha ya kijamii, hapa kuwa na maono ya jinsi unavyogusa maisha ya wengine kwenye jamii. Unajiona jinsi unavyohusiana na wengine na kuendesha maisha yako kwa maono hayo.
Eneo la tatu ni ujuzi unahitajika kuwa nao ili kufanikiwa. Kwa kile unachotaka kufikia kwenye maisha, jua ni ujuzi gani unaopaswa kuwa nao ili kufikia, kisha Jijengee ujuzi huo.
Eneo la nne ni huduma unayotoa kwa wengine, hapa unajiona jinsi ambavyo unatoa huduma yako kwa wengine na wananufaika sana huduma hiyo. Kila hatua unayochukua leo inakuwa na lengo la kukuwezesha kutoa huduma bora zaidi siku zijazo.
Mbili,amua hisia unazotaka kuwa nazo.
Sis binadamu ni viumbe wa kihisia, huwa tunasukumwa kuchukua hatua kulingana na hisia tunazokuwa nazo.
Ili kupata uwazi kwenye maisha yako, lazima uamue ni hisia za aina gani unataka kuwa nazo. Kwa sababu usipoamua hisia unazotaka na kuzitengeneza, dunia itakupa hisia ambazo zitakuwa kikwazo kwako kufanikiwa.
Chagua kuwa na hisia za upendo, furaha, utulivu, amani na epuka kuwa hisia za hofu chuki na wivu.
Tatu, jua kile chenye maana kwako.
Uwazi kwenye maisha unakuja pale unapojua kile chenye maana kwenye maisha yako na kuzingatia hicho.
Kila unachofanya kwenye kazi au biashara, kinapaswa kuendana na maana unayotaka kutengeneza kwenye maisha yako.
Tukutane kesho tujifunze zaidi kuhusu tabia hizi. Yameandikwa na mwanafuzi wa maisha na pia ushauri nasaha.
Maureen Kemei
Blog kufikirichanya.wordpress.com