Habari
Nikukaribishe tuendelee kujifunza kuhusu tabia ya tano leo, kati ya tabia sita, ambazo kocha Brendon Burchard anatushirikisha katika kitabu chake cha high performance habits (how extraordinary people become that way).
Mafanikio yako ni matokeo ya ushawishi wako kwa wengine. Kadiri unavyokuwa na ushawishi kwa wengi ndivyo unavyoweza kufanikiwa zaidi.
Wale wenye ushawishi mkubwa kwenye kazi ndio wanaopata nafasi za kupanda juu zaidi. Wenye ushawishi kwenye biashara ndio wanaopata wateja wengi zaidi. Na wenye ushawishi kwenye maisha yao ndio wanaokuwa na mahusiano bora zaidi.
Njia pekee ya kukuza ushawishi wako kwa wengine ni kuwafanya waone wewe uko upande yao na pia kuwafanya waweze kuwa bora zaidi ya walivyo sasa.
Hatua ya kwanza na muhimu sana kwenye kujenga ushawishi wako kwa wengine ambayo wengi hawatumii ni kuwaomba watu hao wakusaidie kitu. Watu wengi hufikiri ushawishi unatokana na wewe kuwa mwongeaji sana, lakini ukweli ni kwamba ushawishi unatokana na watu kukufikiria wewe mara nyingi. Hivyo unapowaomba watu wakusaidie kitu ata kama ni kidogo wanakufikiria na hivyo unakuwa na ushawishi kwao.
Kuwajali wengine pia kunaongeza ushawishi wako kwao. Zifuatazo ni hatua tatu muhimu katika katika kutengeneza ushawishi wako kwa wengine.
Ushawishi pia unatengenezwa kwa kutoa, pale unapowapa watu kitu bila ya kutegemea kupata chochote, unakuwa na ushawishi mkubwa kwa watu hao. Mtu anapopokea kitu kwako, tena kwa wakati ambao hakutegemea na bila ya kudaiwa kulipa chochote, anamfikiria sana yule aliyempa kitu hicho, na hivyo kuwa ameshashawishika.
MOJA;WAFUNDISHE WATU JINSI YA KUFIKIRI.
Kama utawafundisha watu jinsi ya kufikiri yaani ukiathiri ufikiri wao, unakuwa na ushawishi kwao.
Kuna vitu vitabu ambavyo unapaswa kuwafundisha watu jinsi ya kufikiri, kuhusu wao wenyewe, kuhusu watu wengine na kuhusu dunia kwa ujumla kupitia Kazi unazofanya, hakikisha unawafundisha wengine jinsi ya kufikiri kwa usahihi.
MBILI ;WAPE WATU CHANGAMOTO YA KUKUA ZAIDI.
Unapaswa kuwapa watu changamoto ya kukua zaidi, kutoka pale walipo sasa na kupiga hatua zaidi. Usiwe mtu wa kuwabembeleza watu na kutaka wajione wako vizuri, badala yake kuwa mtu wa kuwaonesha watu ukweli, kwamba wanaweza Kuwa bora zaidi ya walivyo sasa.
Katika kuwasukuma watu wawe bora zaidi, Kuna wengi hawatakuelewa. Wapo ambao watakuona wewe ni mkatishaji tamaa, na wapo wengine wataona ni mtu usiyeridhika. Simamia kuwafanya watu kuwa bora na wale watakaokuwa bora hawatakusahau kamwe.
Yapo maeneo matatu muhimu ya kuwasukuma watu kuwa bora zaidi.
Eneo la kwanza ni kuwasukuma watu kuwa na tabia bora zaidi, kuwafanya wawe waaminifu, wenye uadilifu, wanaojituma na wavumilivu.
Eneo la pili ni kuwasukuma watu ni kwenye mahusiano yao na wengine, kuwafanya waweze kuboresha zaidi mahusiano yao na wengine.
Eneo la tatu ni kuwasukuma watu kwenye mchango wanaotoa kwa wengine, kuwasukuma watoe thamani kubwa zaidi kwa wengine.
TATU ;KUWA MFANO WA VILE UNAVYOTAKA WATU WAWE.
Unaweza kutumia nguvu nyingi sana kuwaambia watu wanapaswa kuwaje, lakini usizae matunda. Lakini wewe unapokuwa kama unavyotaka watu wawe, ujumbe unafika haraka na watu wanakuwa.
Kwa mfano unaweza kuwasisitiza sana watu umuhimu wa kuwahi na usieleweke. Lakini unapoanza kuwa mtu wa kwanza kufika kazini, wale walio chini yako watalazimika kuwahi.
Kile ambacho unataka watu wawe, anza kuwa wewe kwanza na utakuwa mfano mzuri kwao. Watu wanashawishika kwa kukuangalia kuliko kukusikiliza.
Tumejifunza kuwa washawishi wazuri kwa wengine, kwa kuongoza kwa kuwafundisha watu jinsi ya kufikiri, kuwapa changamoto ya kuwa bora zaidi walipo, kuwajali wengine na kuongoza kwa mfano.
Tukutane kesho majaaliwa, makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa ushauri nasaha na mafanikio wa maisha kwa ujumla.
Maureen Kemei.
Blog kufikirichanya.wordpress.com