Karibu, katika uendelezo wa kujifunza kutoka kitabu cha 21 lessons for the 21st century kimeandikwa na Mwana historia Yuval Noah Harari.
Leo tupo changamoto ya nane kati ya 21 ambayo mwandishi ametushirikisha,ambayo inahusu uhamiaji changamoto nyingine kubwa sana katika karne hii.
Tangu enzi na enzi, kumekuwa na mwingiliano baina ya jamii, watu kutoka eneo moja kuhamia eneo jingine. Na mwingiliano huo ndiyo ulioweza kusambaza maarifa na ujuzi katika jamii hizo.
Katika karne ya 21, uhamiaji umekuwa changamoto, baadhi ya mataifa yamekuwa yanaogopa kupokea wahamiaji kutoa kwenye mataifa mengine, wakiamini wahamiaji hao wanaenda kufurahia matunda ya wenzao huku wao wakiwa wameshindwa kutengeneza mazingira bora kwenye nchi zao.
Wale wanaozuiwa kuingia kwenye mataifa wanayotaka kuhamia nao wanayalaumu mataifa hayo kwa ubaguzi wa rangi au dini. Na sehemu kubwa ya watu wanafikiri changamoto kwenye uhamiaji ni rangi au dini. Lakini changamoto kubwa ipo kwenye utamaduni.
Tafiti zote za kisayansi zimeonesha kwamba tofauti yoyote ya kibaolojia baina ya mtu mweusi na mtu mweupe, au mtu wa dini moja na mtu wa dini nyingine. Hivyo tunachotofautiana watu ni utamaduni ambao umejengwa ndani yetu. Tabia tulizonazo ni matokeo ya yale ambayo tumekuwa tunafundishwa na kusisitiziwa tangu tukiwa wadogo.
Hivyo tunapoangalia eneo la uhamiaji, tujue tunasumbuka na utamaduni na siyo rangi wala dini. Pia lazima tukubali kwamba tamaduni zinatofautiana na kila utamaduni una mambo mazuri na mabaya.
Imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio, ushauri nasaha na uandishi.
Maureen Kemei
Blog kufikirichanya.wordpress.com