53/100 . Kutumia tahajudi kuyaelewa maisha.

Karibu, katika kujifunza kutoka kitabu cha 21 lessons for the 21st century ambacho kimeandikwa na Mwana historia Yuval Noah Harari.

Tumeona kwamba njia pekee ya kuyaelewa maisha ni kuelewa mateso ambayo tunayapitia. Lakini watu hawpati nafasi ya kuyaelewa mateso wanayopitia kwa sababu hawana udhibiti wowote kwenye akili zao.

Wengi wanaruhusu akili zao zizurure hovyo bila ya kuelewa kwa nini zinazurura. Mtu anafanya kitu hiki, lakini akili na mawazo yake yapo kwenye kitu kingine.

Na pia inapotokea mtu anakutana na ugumu au changamoto, akili haipendi kukaa kwenye ugumu ule, badala yake inahama na kwenda kwenye vitu ambavyo siyo vigumu na wala siyo changamoto. Kwa njia hii inakuwa vigumu mtu kuyaelewa mateso na kuyaelewa maisha.

Jawabu la changamoto hii ni mtu kufanya tahajudi, kutenga muda kwenye siku ambao unaitumia kuangalia akili yako jinsi inavyohangaika na kuzurura. Tofauti na wengi wanavyofikiri kwamba tahajudi ni kudhibiti akili, hapa unatumia tahajudi kuiangalia akili, na kuona namna inavyozurura.

Njia rahisi ya kufanya tahajudi ni kukaa eneo tulivu, kufunga macho yako na kuielekeza akili yako kwenye pumzi zako, unapovuta pumzi ndani fikiria unavuta pumzi ndani, unapoitoa nje fikiria unatoa pumzi nje.

Akili yako inapohama kutoka kwenye pumzi zako na kwenda kwenye mengine ona hilo kwamba akili yako imehama. Ni zoezi rahisi kwa kusoma hapa, lakini jaribu kufanya na hazitapita sekunde kumi akili yako itaanza kuhangaika na vitu vingi kuliko unavyoweza kufikiri.

Tahajudi ndiyo njia pekee tunayoweza kuitumia kujijua sisi wenyewe na baada ya kujijua kuweza kupiga hatua zaidi kiutambuzi. Tahajudi ndiyo zana pekee tuliyonayo ambayo inaweza kutusaidia tusizidiwe utambuzi na maendeleo makubwa yanayotokea kwenye teknolojia, hasa ujio wa maroboti.

Hatua za kuchukua.

Tutenge muda wa kufanya tahajudi kwenye kila siku ya maisha yetu. Mwandishi anasema amekuwa akifanya tahajudi katika kila siku ya maisha yake.

Hilo limemsaidia kuandika vitabu mbalimbali ambavyo vimekuwa na mchango mkubwa sana kwenye maisha ya mwanadamu.

Ahsante kwa kusoma nakala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio, ushauri nasaha na uandishi.

Maureen Kemei.

Blog:kufikirichanya.wordpress.com

Maisha yangu, uchaguzi wangu.

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *