Karibu.
Tofauti yetu sisi binadamu na viumbe wengine ni uwezo wetu wa kupangilia mambo yajayo. Tuna uwezo wa kufikiri na kutengeneza taswira yoyote kwa mambo yajayo. Ni pale uwezo huo unapotumika vibaya, ambapo mtu anatengeneza taswira mbaya ndipo hofu na wasiwasi huzaliwa.
Sehemu kubwa ya vitu ambavyo huwa tunavihofia huwa havitokei. Na hata pale vinapotokea madhara yake huwa siyo makubwa kama vile tuliyokuwa tunahofia. Hivyo hiyo inatosha kusema kuwa hofu na wasiwasi ni matumizi mabaya ya uwezo mkubwa ulio ndani ya kila mmoja wetu.
Kwenye kitabu cha breakfast with Seneca by David Fideller, Seneca anaeleza kuwa kuna hofu kubwa mbili zinazowasumbua wengi, ambazo ni hofu ya kifo na hofu ya umaskini au tamaa ya utajiri.
Hatua ya kwanza ya kukabiliana na hofu ambayo Seneca anafundisha ni kujua kwamba Kuna mambo yapo ndani ya udhibiti wetu na mengine yapo nje ya udhibiti wetu. Hivyo tunapswa kujua yaliyo ndani ya uwezo wetu na kuyafanyia kazi na yaliyo nje ya uwezo wetu kuyakubali jinsi yalivyo.
Hatua ya pili ni kuwa na tafsiri sahihi ya mambo yanayotokea. Mambo huwa yanatokea kwa namna yanavyotokea. Tafsiri kwamba mambo ni mazuri au ni mabaya ni sisi wenyewe tunatengeneza. Hivyo kwa kuacha kuweka tafsiri mbaya kwenye mambo yanayotokea kunasaidia kupunguza hofu na wasiwasi. Ukiacha kujiambia umeumizwa, dhana ya maumivu haipati nafasi kwako.
Hatua ya tatu ni kuishi kwenye wakati ujao. Kama tulivyoona hofu na wasiwasi ni zao la taswira tunazozijengea kwenye wakati ujao. Kama tukiacha kuhangaika na wakati huo ujao na kuishi kwenye wakati uliopo, tutapunguza sehemu kubwa ya hofu na wasiwasi.
Tuchukue hatua sasa, tuna uwezo mkubwa wa akili zetu zinazotuwezesha kukabiliana na yale yaliyo mbele yetu, sasa badala ya kuhangaika na yajayo ambayo hatujayafikia. Tunapaswa kuhangaika na yale tunayomiliki kwa sasa yale tu ambayo yapo ndani ya udhibiti wetu.
Uwe na wakati mwema na #fikrachanyakilasaa .
Akujaliaye, Mwandishi.
Maureen Kemei.
Blog, kufikirichanya.wordpress.com