Kikwazo kikubwa kinachofanya watu kushindwa kuishi maisha halisi ni kutokujitambua na hivyo kujikuta wakiiga watu wengine.
Hii imekuwa hatari sana kwenye zama hizi ambapo ushauri wa maisha umekuwa mwingi. Wengi wanajikuta wakiiga wengine kwa namna mbalimbali hivyo licha ya kuweka juhudi na muda bado hawafanikiwi. Ni muhimu kujitambua wewe mwenyewe hili ushi maisha halisi kwako.
Kwenye Ustoa, Kuna vitu vinne muhimu ambavyo mtu anapaswa kuvijua kuhusu yeye mwenyewe ili aweze kujitambua na kuishi maisha halisi kwake.
Kitu cha kwanza ni asili yetu kama binadamu. Sisi binadamu tuna asili inayotutofautisha na viumbe wengine wote hapa ulimwenguni. Na uwezo wetu kubwa ni kuweza kufikiri na kufanya maamuzi. Hicho ni kitu kinachopatikana kwa binadamu pekee na chenye nguvu kubwa. Lazima ujue asili hii na uweze kuitumia ili kuishi maisha halisi kwako. Kila mara ni vizuri kutulia na kujiuliza kama umefikiri vizuri na kufanya maamuzi au umefuata tu mkumbo. Wanyama huwa wanafuata mkumbo, wewe usiwe kama wao.
Kitu cha pili ni uwezo wa vipaji uivyonavyo, kila mtu ana uwezo wa kipekee na mkubwa sana ambao amezaliwa nao. Uwezo ambao hauwezi kupatikana kwa mtu mwingine yoyote. Na kila mtu ana vipaji vyake, vitu anavyoweza kuvifanya vizuri na kwa upekee mkubwa.
Jua uwezo wako na vipaji vyako na kuvitumia, maana iyo ndiyo njia pekee ya kuishi maisha halisi kwako. Uzuri ni kwamba uwezo mkubwa na vipaji vyetu huwa havipotei, vinabaki na sisi maisha yetu yote.
Kitu cha tatu ni bahati tunazokutana nazo kwenye maisha. Kuna mambo mengi yanayotokea kwenye maisha ambayo hayapo ndani ya udhibiti wako. Hayo yote huwa yanakuja na fursa nzuri ambazo ukiweza kuzitumia utaishi maisha halisi kwako. Bahati zinaweza kuwa eneo uliozaliwa, elimu uliyopata, watu unaokutana nao na kadhalika. Tangu umezaliwa mpaka sasa umepitia mambo mengi ambayo ukiweza kuyatumia vizuri utaishi maisha halisi.
Kitu cha nne ni utashi wetu ambao unabebwa na kusudi na ndoto tunazokuwa nazo. Yale unayochagua kufanya kwenye maisha yako, ambayo yanatokana na msukumo ulio ndani yako yanakufanya uishi maisha halisi kuliko yale unayoiga. Hivyo ni muhimu sana ulijue kusudi lako na uwe na ndoto kubwa zinazotoka ndani yako hili kuwa na maisha halisi kwako.
Chukua hatua, Ustoa unasisitiza sana tujitambue sisi wenyewe ili tusisumbuke na mambo yasiyo sahihi kwetu. Maana Kuna watu wengine wanaweza wakafanya na wakafanikiwa vizuri, ila wewe na mimi tunaweza tukafanya na tusifanikiwe.
Ili kuepuka kupoteza muda na nguvu, tujitambue na kuishi kulingana na upekee na utofauti wetu. Kuiga maisha ya wengine ndiyo chanzo cha wengi kuwa na maisha magumu.
Wako akujaliye sana.
Maureen Kemei.
Blog, kufikirichanya.wordpress.com
Uwe na siku njema na # sambaza uchanya.