Katika maisha yetu kila anayeumia ana mtu wa kumlaumu, na huwa hawakosekani. Kila anayeshindwa kwenye maisha ana watu wa kuwatupia lawama, na hawakosekani.
Kila mara hasa kipindi hiki unasikia watu wakisema utawala ni mbaya, uchumi mbovu, maisha yamekuwa magumu sana kila kitu kimepanda. Wazazi wamelegea kwenye malezi na hata mazingira siyo rafiki sana.
Lakini, ukweli ni kwamba, kwenye kila sababu ambayo mtu anatoa, kuna wengine wamepitia hali hiyo hiyo ila wakafanikiwa sana.
Hivyo, unapaswa utambue ya kwamba, upo hapo ulipo siyo kwa sababu ya mtu mwingine yeyote, bali wewe mwenyewe. Imani, mtazamo ambazo umekuwa nazo ndizo zimekufikisha hapo ulipo, kwa hivyo hupaswi kamwe kulaumu mtu yeyote ule.
Na wewe mwenyewe ndiye utakayejitoa hapo ulipo sasa. Chochote unachokilaumu sasa kwamba kinakuzuia usifanikiwe, hebu jaribu kuangalia hadithi za wengine waliopita hali kama zako na wakafanikiwa sana.
Hili siyo ikupe tu hamasa, bali ikupe nguvu ya kuachana na sababu unazojipa. Ukiachana na sababu hizo utaweza kuona fursa na hivyo kuchukua hatua za kimaendeleo badala ya kulaumu.
Hatua ya kuchukua, anza sasa kujua kwamba ni wewe mwenyewe unayejizuia kufikia mafanikio makubwa. Usijipe sababu ya kutofanya jambo, bali unafanya kwa sababu unajua ni wewe unawajibika na maisha yako.
Akujaliaye sana.
Maureen Kemei.
Blog, kufikirichanya.wordpress.com