Watu wengi kwenye zama hizi hutamani kupata utulivu wa kiroho, kimwili, kihisia na maisha kwa ujumla. Lakini wengi bila kujua hujikuta wakitafuta utulivu huo huko nje.
Watu wengi huhangaika na mambo ya nje ili kujaza shimo lililo ndani yao, kitu ambacho huwa hakiwezekani. Wapo watu wanahama dini, kazi, ndoa, mahusiano na vitu vingine, lakini kule wanakoenda wanagundua hakuna kipya ukilinganisha na walikotoka.
Utulivu wa kweli ni ule unaojitafutia mwenyewe, utulivu wa ndani, unaamua kujitenga na ulimwengu wa kelele mingi na kutumia muda huo kuyatafakari maisha yako.
Unapotafari hivyo unaafikiana na nafsi yako, yaani unaongea na wewe mwenyewe, kwa kufanya hivyo utajua ni wapi una madhaifu na kuweza kuiboresha. Na pale unapoenda vizuri unajipongeza na kutia bidii zaidi.
Kwa kufanya hivyo unapata utulivu wa ndani, na utaachana na kuhangaika na mambo ya nje. Hutakwazika wala kuumizwa na watu wanapokusema vibaya maana unajijua mwenyewe.
Hatua ya kuchukua, jitafakari mwenyewe kama unafuata mambo ya nje, watu wanasema nini juu yako, ama unajielewa mwenyewe, unakuwa na muda wako wa kujitenga kisha kujihoji mwenyewe.
Kwa kujihoji hivyo, unaweza kujirekebisha na kuweza kusonga mbele zaidi bila msongo wowote.
Akujaliye sana.
Maureen Kemei.
Blog, kufikirichanya.wordpress.com