Njia 10 za kutengeneza tabia za furaha.

Kila ambaye amekuwa anaanza kufanya kitu chochote kwenye maisha yake kwa lengo la kupata furaha amekuwa anaishia kujisikia vibaya baada ya kupata alichofikiri akipata kitampa furaha.

Wengi wetu tunapokutana na hali hii huwa tunafikiri kuna shida kwenye kile tunachopata. Lakini ukweli ni kwamba shida haipo kwenye chochote tunachotaka, bali shida ipo ndani yetu.

Furaha ya kweli kwenye maisha huanza ndani, ni kitu kinachoanzia kwenye fikra zetu na siyo matokeo ya kile tunachopata. Hata kama tumepata kitu kikubwa na muhimu kiasi gani, furaha yake huwa ni ya muda mfupi tu, baada ya hapo tunarudi kwenye hali yetu ya kawaida.

Kutoka kwenye kitabu cha “habits of a happy brain,”Loretta Graziano Breuning anatushirikisha njia kumi za kutusaidia  kutengeneza tabia za furaha kwenye bongo zetu.

Wote tunajua kwamba mabadiliko huwa yanakuwa magumu kwa sababu ya tabia. Tabia mpya huwa ni ngumu kujijengea, na tabia za zamani huwa ni ngumu kuzivunja. Bila ya kuwa na njia sahihi, zoezi la kutumia ubongo wetu kuzalisha furaha litakwama.

Moja, jifunze kwa wengine, angalia watu ambao wana tabia unazotaka kujijengea kisha jifunze wanafanya nini na wewe ufanye. Ukifanya kile ambacho wenye furaha wanafanya, na wewe utakuwa na furaha pia.

Mbili, tumia kemikali za furaha ambazo hutumii kwa sasa. Kila mtu kuna kemikali anazotumia sana na ambazo hatumii kabisa. Ili kutengeneza tabia za furaha, angalia ni kemikali zipi hutumii na anza kuzitumia. Kama umekuwa mtu wa kuweka malengo na kuyafikia, kazana pia kuboresha mahusiano yako na wengine na hilo litakupa furaha.

Tatu, tengeneza tabia mpya kwenye tabia za zamani ulizonazo sasa. Angalia kile kitu ambacho unapenda kukifanya sasa, kisha ona jinsi gani unaweza kukifanya na ile tabia unayotaka kujenga. Unapohisianisha vitu hivi viwili unaweza kujenga tabia bora kwako.

Nne, nguvu. Kujenga tabia yoyote kunahitaji nguvu, hivyo panga kufanya kile unachofanya ili kujenga tabia mpya unapokuwa na nguvu. Asubuhi na mapema ni muda mzuri wa kufanya yale yanayojenga tabia mpya.

Tano, sifa. Unapofanya kitu kwa ajili ya sifa yako ya baadaye inakuwa rahisi kwa kitu hicho kuwa tabia. Pale unapofikiria kuacha alama fulani hata baada ya kuondoka, unasukumwa kufanya zaidi.

Sita, burudani. Fanya zoezi la kujenga tabia mpya kuwa burudani kwako. Usifanye kama ni jukumu zito na linalochosha, badala yake fanya kuwa burudani na itakuwa rahisi kwako kuendelea nalo.

Saba, vunja jukumu kubwa kwenye majukumu madogo madogo, na unavyokamilisha sehemu ndogo ya jukumu unapata hamasa ya kuendelea na jukumu sehemu nyingine. Kwa kugawa majukumu madogo madogo haikuchoshi wala kukukatisha tamaa.

Nane, fanya inayoridhisha badala ya kutaka kufanya iliyo kamili. Badala ya kusubiri mpaka uweze kuchukua hatua iliyo kamili na sahihi zaidi, chukua hatua inayoridhisha. Unapoona nafasi ya kuchukua hatua, hata kama haijakamilika, ni bora kuliko kusubiri mpaka upate ukamilifu ambao haupo.

Tisa, anza maandalizi mapema. Unapojua kuna tabia unataka kujijengea, anza maandalizi yake mapema kabla ya kufika wakati unaohitaji.

Kumi, tengeneza taswira ya kuwa na ile tabia unayotaka kutengeneza. Kwa kutengeneza taswira ya aina hiyo, njia zako kwenye ubongo zinazotengeneza tabia zinaimarika hata bila ya kufanya tabia husika. Hii limedhibitishwa na tafiti kwenye michezo, wachezaji ambao wanatengeneza taswira wakiwa wanacheza vizuri wanaimarisha uchezaji wao hata kama hawajacheza.

Hatua ya kuchukua, rafiki, tutumie njia hizi kumi katika kujijengea tabia za furaha ambazo zitadumu kwenye maisha yetu. Tuiaje kukimbilia njia za kupata furaha kwa haraka na pia furaha hizo huishia kuwa huzuni baadae.

Akujaliaye sana.

Maureen Kemei.

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *