Ubongo wetu ni rahisi sana kusumbuliwa, tunapokuwa tunafanya kazi, kitu chochote kipya kinachotokea, ni rahisi kututia kwenye kile tunachofanya na kujihusisha na kitu hicho kipya. Ndiyo maana ni vigumu sana kufanya kazi muhimu ukiwa kwenye eneo lenye kelele, akili yako haiwezi kutulia kwenye kile unachofanya.
Kuna usumbufu wa nje, ambao unatokana na vitu vipya vya nje ambavyo ubongo unashawishika kujihusisha navyo. Simu zetu za mkononi ndiyo chanzo kikuu cha usumbufu wa nje. Tafiti nyingi zinaonesha watu hawawezi kukaa kwa zaidi ya dakika kumi bila kuangalia simu zao, kitu ambacho kinawazuia kuweka umakini kwenye kazi zao.
Hivyo kama unataka kuwa na ufanisi mzuri, pale unapokuwa unafanya jukumu muhimu, zima kabisa simu yako. Au iweke kwenye ukimya na ikae mbali kabisa na wewe. Pia fanya kazi zako eneo ambalo halina usumbufu wa watu wengine au makelele.
Aina ya pili ya usumbufu ni usumbufu wa ndani, hapa akili yako mwenyewe inakuwa inahama hama kutoka kwenye kitu kimoja na kwenda kwenye kitu kingine. Kama hutaweza kuidhibiti akili yako na kuiweka kwenye kile unachofanyia kazi, utajikuta unachoka sana lakini haikamilishi unachofanya.
Njia bora ya kuondokana na usumbufu huu ni kujikamata pale mawazo yako yanapotaka kuhamia na kuyarudisha kwenye kile unachofanya. Ukichelewa kujikamata na ukajikuta mawazo yameshahamia sehemu nyingine, inakuwa kazi kubwa kuyarudisha kwenye kazi kuu.
Hatua ya kuchukua, kuwa mlinzi wa mawazo yako na yakamate pale yanapotoroka na uyarudishe kwenye jukumu kuu.
Akujaliaye sana
Maureen Kemei.