Hitaji letu la kuharakisha kila kitu limekuwa kikwazo kwenye mambo mengi kwa sababu hatukubali ukomo tulionao.
Tunaamini kwa sababu teknolojia inaharakisha viti vingi, basi kila kitu kinaweza kuharakishwa.
Lakini kuna vitu vingi kwenye maisha ambavyo hakuna namna unaweza kuviharakisha, hata ufanyeje.
Kutoka kwenye kitabu cha four thousand weeks na Oliver Burkeman. Anatushirikisha vitu ambavyo hatuwezi kuharakisha kwenye maisha.
Moja ya vitu hivyo :ni usomaji wa vitabu. Watu wamekuwa wanalalamika kwamba hawana muda wa kusoma vitabu. Lakini watu hao wanatumia muda mwingi kwenye mitandao na mambo mengine.
Ambacho hawataki kukubali watu hao ni kwamba hakuna namna unaweza kuharakisha usomaji. Unaweza kuharakisha kuperuzi mitandao ya kijamii, kwa kupita haraka haraka kwa kasi kubwa.
Lakini huwezi kuharakisha usomaji wa kitabu na ukatoka ukiwa umeelewa vizuri ulichosoma. Unahitajika kutenga muda wa kutosha na wa kusimama na kusoma kwa umakini na utulivu mkubwa. Kitu ambacho ni adimu sana kwenye zama hizi za kasi ya teknolojia na kukosa subira.
Kusoma kitu kwa namna ambayo utakielewa na kunufaika nacho kunahitaji muda wa kutosha na hakuna namna ya kuharakisha hilo.
Watu wamekuwa wakijaribu usomaji wa kasi, lakini uelewa umekuwa ni ndogo. Pia watu wamekuwa wakijaribu kusikiliza vitabu vilivyosomwa, nako pia uelewa unakuwa mdogo.
Katika kuendeleza ukosefu wa subira na kutaka kuharakisha vitu, watu wamekuwa wanasikiliza vitabu vilivyosomwa kwa kasi mara mbili ya kawaida. Hapo wanaona wanajifunza mengi kwa muda mchache,lakini ni kujidanganya tu, kwani uelewa kwao unakuwa ni mdogo sana kwenye kasi ya aina hiyo.
Hatua ya kuchukua, kwa kukubali kwamba tumenaswa kwenye uraibu wa kufanya mambo kwa kasi, ambayo haileti utija kwenye maisha yetu, yatatusaidia tuchukue hatua ya kutenga muda wa kutosha na wenye utulivu wakati wa kusoma au kufanya jambo muhimu.
Akujaliaye sana.
Maureen Kemei