Hakuna kitu kinachowaangusha wengi kama kujilinganisha na wengine. Kwa sababu haijalishi umepiga hatua kiasi gani, Kuna mtu mwingine ambaye amepiga hatua zaidi yako.
Ukianza kujilinganisha na watu, utaingiwa na wivu kwa kuona wamekuzidi na hilo litaathiri mahusiano yako na watu hao.
Sisi binadamu huwa hatuwezi kuficha hisia zetu, hivyo hisia zozote ulizonazo kwa wengine huwa zinajiweka wazi unapokuwa nao. Hivyo hata kama utaficha kiasi gani bado watu watajua hisia ulizonazo juu yao.
Kuepuka hilo, acha kujilinganisha na yeyote, mpende na kumheshimu kila mtu ukijua kila mtu yuko kwenye njia yake ya maisha.
Muhimu zaidi usiwachukie wale waliofanikiwa kuliko wewe. Kwenye jamii nyingi matajiri wamekuwa wakipewa majina mabaya na kuonekana ni watu wabaya, hakikisha huingii kwenye mkumbo huo.
Ukiwachukia matajiri kamwe huwezi kuwa tajiri, hivyo wapende wale waliofanikiwa kuliko wewe, wapende kweli kutoka ndani yako na hilo litakufanya uwe tayari kujifunza kutoka kwao na wewe uweze kufanikiwa pia.
Hatua ya kuchukua ;ondokokana kabisa na fikra na hisia zozote hasi, hizo ni kikwazo kwako kufanikiwa. Mara zote kuwa na hisia na fikra chanya ambazo zitakusukuma kufanikiwa zaidi.
Akujaliaye sana.
Maureen Kemei.