Kila mmoja huwa ana nyakati za furaha na huzuni. Kila mtu huwa ana matatizo mbalimbali, yanaweza kuwa ya fedha, kazi, biashara, familia, mahusiano na mengine mengi.
Watu wengi hutumia matatizo wanayokutana nayo kwenye maisha kama sehemu ya kulaumu, kulalamika na kutafuta huruma kutoka kwa wengine. Huwa tayari kuwaambia wengine matatizo yao kwa kuona kama ndiyo matatizo makubwa kuliko ya wengine wote.
Kufanya hivyo siyo sahihi kwa sababu kubwa mbili. Moja ni kila mtu ana matatizo yake na ya wengine yanaweza kuwa makubwa kuliko ya kwako. Na mbili ni matatizo yako ni yako, hayawahusu wengine, hakuna anayejali sana kuhusu matatizo yako.
Joe Girard anatushirikisha kwenye kitabu chake cha “Girard’s 13 essential rules of selling,” kwamba kitu pekee kitakachoweza kukuvusha kwenye nyakati unazopitia magumu na matatizo mbalimbali ni kuwa na mtazamo chanya.
Ni wakati huo wa magumu ndiyo unapaswa kuwa imara sana kwani ndiyo wakati rahisi kwa mtu kuyumba na kuanguka. Wakati mambo ni mazuri kila mtu anaweza kufanya vizuri, ni nyakati ngumu ndizo wengi wanashindwa.
Kuwa na mtazamo chanya wakati unapitia magumu ni muhimu kwa sababu Kuna wakati utakuwa na wasiwasi na wewe mwenyewe. Kuna wakati utakuwa na mashaka na maamuzi uliyofanya, utaona kama unakosa. Hiyo ni hali ambayo ni lazima utaipitia kama binadamu. Kitu pekee kitakachokuwezesha kuendelea licha ya kukutana na hali hiyo ni mtazamo chanya unaokuwa nao.
Mtazamo chanya ndiyo unaowatofautisha wale wanaofanikiwa na wanaoshindwa. Kufanikiwa kwenye maisha ni matokeo ya kuweza kukabiliana na nyakati ngumu na kuzivuka. Mtazamo chanya wa kifikra unakupa nguvu ya kuvuka chochote na kuendelea bila ya kukata tamaa. Hata kama hujapata matokeo unayoyataka, unapokuwa na mtazamo chanya unajua una wakati mwingine wa kufanya kwa ubora zaidi. Hukati tamaa kwa kuona ndiyo mwisho, bali unajua ni sehemu ya safari lazima iendelee.
Hatua ya kuchukua, mara zote kuwa na mtazamo chanya na ya uwezekano. Fanya kila anayekutana na wewe ajue upo chanya, usiwe mtu wa kulaumu, kulalamika au kulia lia shida zako kwa wengine. Kwa kuonekana ukiwa chanya mara zote kunawafanya watu wakuamini na kushawishika na wewe.
Yeyote unayemwona amefanikiwa, kuwa na uhakika kwamba safari yake halikuwa rahisi. Amepitia mengi magumu ambayo yalimkatisha tamaa. Kilichomwezesha yeye kufanikiwa ni kuwa na mtazamo chanya wa kiakili. Kama na wewe unataka kupata ushindi na mafanikio kwenye maisha yako, hakikisha unakuwa na mtazamo chanya wa kiakili mara zote.
Kuwa na mtazamo chanya ni silaha ya wale wanaoshinda matatizo na magumu kama ambavyo tumejifunza. Uwe na simu njema.
Mimi wako akujaliaye sana.
Maureen Kemei.