Umuhimu wa kuwa na subira.

Mambo mazuri huwa hayataki haraka, hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio kama unataka mafanikio makubwa, lazima uwe na subira.

Wengi wetu tunashindwa kwenye hii safari kwa sababu tuna haraka ya kupata mafanikio, hasa vijana wa kisasa wengi wetu tunataka kumaliza shule leo, kuajiriwa na kupata bosi mzuri leo, kazi kusiwe na changamoto yoyote, tujenge nyumba nzuri leo na tuolewe au kuoa na ndoa kusiwe na changamoto yoyote.

Matarajio haya hayawezekani, lazima changamoto, maumivu na magumu katika maisha ya mwanadamu yatokee. Lazima tujifunze namna ya kuwa na subira kwa kile tunachofanya au tunachopitia.

Mtu yeyote anayejua kile anachotaka, na ambaye yuko tayari kuweka kazi kukipata, ni swala la muda tu, akiwa na subira, ung”ang”anizi na uvumilivu,lazima atapata anachotaka.

Kitu muhimu tunachopaswa kujua ni kwamba, mambo huwa yanatokea kwa wakati wake yenyewe, siyo kwa wakati tunaopanga wenyewe. Chochote tunachotaka tutakipata kwa wakati wake, lakini haitakuwa wakati tunaopanga sisi.

Hivyo tusione tunachelewa kupata tunachotaka na kukata tamaa, kuwa na subira, tuendelee kukaa kwenye mchakato na wakati sahihi utakapofika, tutapata tunachotaka.

Ili tuweze kuwa na subira, tunapaswa kuacha kuhesabu na kufanya sehemu yetu. Tuweke mkazo kwenye mchakato na siyo matokeo au muda ambao tumeweka juhudi. Kadiri mchakato na muda unavyokwenda, ndivyo tunavyojiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata kile tunachotaka.

Kila mtu anataka kupata utajiri wa haraka na kwa njia za mkato, lakini dunia huwa ina namna yake sahihi ya kukamilisha mambo, huwezi kuilazimisha bila ya kuleta madhara. Ni lazima uweke juhudi na muda ndiyo dunia ifike hatua ya kukupa kile unachotaka.

Na kama ambavyo tumeshaona, lazima tuwe na ujuzi maalumu na tujijengee jina na sifa nzuri. Lazima tuwe bora kabisa kwenye kile tunachokifanya, tuweke juhudi na kujipa muda na mwisho tutapata matokeo makubwa.

Hatua ya kuchukua, penda unachofanya na ukifanye kwa sababu unakipenda. Hilo litakufanya uwe na subira na uendelea kufanya, bila kuangalia muda au matokeo.

Wako akujaliaye sana.

Maureen Kemei.

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *