Kila mmoja wetu huwa ana sauti ya kukatisha tamaa ambayo ipo ndani yake. Ni sauti hiyo ndiyo huwa kikwazo kwa wengi kufanya makubwa.
Hakuna asiyeweza kuijua ni nini anapaswa kufanya ili apate anachotaka. Ila wakati wa kufanya kitu hicho unapofika, sauti ya ndani inawashawishi na wanaishia kutokufanya.
Kwa mfano unaweza kuipanga vizuri kabisa kwamba kesho utaamka asubuhi na mapema. Unaweka kabisa alamu kwenye simu yako kwamba muda ukifika ikuamshe.
Muda unafika, alamu unaita, unaisikia kabisa, lakini sauti ya ndani inaanza hadaa yake. Sauti hiyo inakuambia ulale kidogo ndiyo uamke, inakushawishi kwamba jana ulichoka sana. Inakuhadaa kwamba unahitaji dakika tano tu za ziada za kulala halafu utaamka.
Unajua unapoisikiliza sauti hiyo, unakuja kuamka saa moja au mawili baadaye, umeshachelewa na mipango uliyokuwa umeweka uikamilishe mapema inakuwa haiwezekani tena.
Bila kuiua sauti hiyo ya ndani utapanga, mambo mengi sana, lakini hakuna lolote utakalokamilisha. Maana sauti hiyo haitaki kukuona ukiteseka, itatumia kila ushawishi kuhakikisha husumbuki na mambo makubwa.
Sauti hiyo ya ndani ipo ndani ya kila mtu, tumekuwa nayo kwa miaka yetu yote. Ni sauti yenye nguvu kubwa ya ushawishi kwetu, kwa sababu inajua sana udhaifu wetu.
Inabidi ujue sauti hiyo kwa sababu ukiiacha hai, huwa haichoki, Itaendelea kukushawishi na hasa kukukamata kwenye udhaifu wako na hapo utajikuta umehadaika na sauti hiyo ya ndani na kutokufanya kile unachojua ni muhimu kufanya.
Kuijua sauti hiyo unapaswa kutaka sana kile unachotaka kiasi kwamba hakuna namna utakwamishwa na chochote. Macho yako na umakini wako wote unakuwa kwenye kile unachotaka kiasi kwamba mengine yote yanakosa maana kwako.
Hatua ya kuchukua, unapaswa kuwa bize sana na kile unachotaka kiasi kwamba sauti hiyo ya ndani inakosa kabisa nafasi. Kila inapotaka kuja kwako hakuna mahali inapata nafasi.
Msukumo wako kwenye kile unachotaka unakuwa mkubwa mno kiasi kwamba hakuna chochote kinachokuyumbisha. Unachokuwa unataka ni kile unachotaka na hakuna kingine chenye nafasi.
Akujaliaye sana.
Mwandishi wako.
Maureen Kemei.