Kosa kubwa ambalo watu wengi wanalifanya kwenye siku zao ni kupoteza muda na nguvu kwenye mambo yasiyo na tija.
Wengi wanafanya kazi au biashara ambazo hawazipendi. Hivyo wanachelewa kuanza kazi na kuwahi kumaliza.
Lakini pia wakati wa kufanya, wanaingiliwa na usumbufu mwingi kitu ambacho kitu kinachofanya ufanisi wao kuwa mdogo. Kwa kifupi japo mtu huyu anakuwa kwenye kazi, hatumii nguvu zake zote kwenye kile anachofanya.
Lakini sasa, siku ya kazi inapoisha anajiambia amechoka na hawezi kufanya kitu kingine. Haangalii masaa mengine nje ya hiyo ya kazi, ambayo ni mengi kuliko yale ya kazi.
Ufanyaji kazi wa wengi siyo wenye tija kwamba kuna matokeo anataka kuzalisha. Mtu anafanya tu ili amalize au muda uende. Pamoja na kufanya kazi mbovu kwenye theluthi moja ya muda wake, bado anapoteza theluthi nyingine mbili.
Kama mtu anataka kweli kuishi kwa ukamilifu na kufanya makubwa, ni lazima atengenese siku ndani ya siku, yaani awe na siku mbili ndani ya siku moja.
Siku ya kwanza ni ile ya kazi inayoanza saa mbili asubuhi mpaka saa kumi jioni. Na siku ya pili ni ile binafsi nje ya kazi inayoanza saa kumi jioni mpaka saa mbili asubuhi.
Siku ya kwanza ambayo ni ya kazi ina masaa 8,siku ya pili ambayo ni binafsi ina masaa 16. Unaweza kujionea hapo kwamba kila mtu ana muda mwingi nje ya muda wa kawaida wa kazi au biashara.
Wengi hupoteza hayo masaa ya nje ya kazi wakijiambia wanapumzika. Lakini ukweli ni kwamba kazi za wengi ni za kutumia akili kuliko nguvu na akili huwa haipumziki, bali inabadili vitu vya kufanya hili kuondoa hali ya uchoshi.
Hatua ya kuchukua akili haichoki kama misuli, hivyo tofauti na kulala haihitaji mapumziko, bali inahitaji mabadiliko. Ukifanya kitu kimoja kwa muda mrefu akili inakichoka.
Ukikiacha hicho na kufanya kitu kingine akili inakuwa na nguvu za kutosha, hata kama ni kitu kigumu.
Akujaliaye sana.
Mwandishi, Maureen Kemei.
Fikrachanya.wordpress.com