Kutoka kwenye kitabu cha ‘the third door ‘ Alex Banayan anatushirikisha jinsi alivyokutana na wanamafanikio mbalimbali kwenye safari yake ya kutaka kujua nini kiliwafanya wafanikiwe.
Baada ya Alex kuhakikishwa mahojiano na Warren Buffett,Alex aliomba kabla hajatuma barua hiyo ajiandae kwanza Ili atakapopata nafasi atumie vizuri.
Alienda kusoma kila kitu kinachomhusu Warren Buffett. Alikusanya vitabu 15 vya wasifu wa Warren Buffett,na mafunzo mengine yanayomhusu . Mchana alikuwa anasoma vitabu,jioni anasikiliza sauti na usiku anaangalia video za Warren.
Katika kipindi hicho alichota busara nyingi sana kutoka kwa Warren Buffett kupitia maarifa aliyopitia yanayomhusu. Aliweza kupata majibu ya changamoto ambazo yeye na hata marafiki zake walikuwa wanapitia.
Alijifunza jinsi Warren Buffett alivyoanza biashara akiwa na umri wa miaka 6. Alijifunza jinsi alivyoanza uwekezaji mapema na kuwa dalali wa soko la hisa.
Wakati anaanza ilikuwa vigumu kupata mkutano na matajiri aliolenga kuwauzia hisa. Hivyo alitafuta ushawishi mzuri zaidi ambapo aliwaambia ana njia ya kuwasaidia kupunguza kodi wanayolipa na hapo kila mmoja alikuwa tayari kukutana naye.
Hapo alijifunza kwamba watu wanaweza kukataa kukutana na wewe kwenye kile ulicholenga,lakini kuna kitu wanachohitaji,ukiweza kukijua na kuitumia,watakubali kukutana na wewe.
Pia alijifunza umuhimu wa kuchagua kazi inayokupa ujuzi na uzoefu kuliko inayokulipa sana. Wakati Warren anahitimu shahada yake ya uzamivu kwenye biashara (MBA ). Alikuwa na fursa ya kupata kazi ambayo ingemlipa sana. Lakini yeye hakufanya hivyo,aliomba kufanya kazi kwa aliyekuwa mwekezaji maarufu na mwalimu wake Ben Graham.
Kwa miaka miwili maombi yake yalikataliwa,hata alipokuwa tayari kufanya kazi bure bado alikataliwa. Lakini kwa ung’ang’azi wake alifanikiwa kupata kazi hiyo.
Alifanya kwa miaka miwili na kujifunza mengi na Graham alipostaafu, Warren alienda kuanzisha kampuni yake ya uwekezaji na wateja wote wa Graham wakawa wake.
Alex aliwasimulia marafiki zake yale yote aliyojifunza kwa Warren na mara zote walipata majibu ya changamoto zao. Na wote walimchukulia Warren kama babu yao na kutegemea sana busara zake katika maisha yao .
Kuchukua hatua, Warren Buffett ni mfano mzuri kwetu tukijifunza kutoka kwake tutaweza kuwekeza na kufanya biashara kwa mafanikio makubwa,bora tu tuwe tayari kujifunza na kuchukua hatua.
Akupendaye sana.
Mwandishi Maureen,
www.uamshobinafsi.com.