Namna ya kuwa mghairishaji mzuri.

Kujifunza kuwa mghairishaji mzuri ni rahisi,lakini kutekeleza siyo rahisi. Hapa kuna msingi ya kuzingatia ili kuweza kutekeleza hilo.

Msingi wa kwanza ni kujilipa mwenyewe. Huu ni msingi muhimu sana kwenye eneo la fedha,kwamba unapopokea fedha,ukianza kujilipa mwenyewe kwa kuweka akiba halafu ndiyo matumizi yakafuata,utakuwa na akiba.

Lakini ukianza na matumizi kwa kutegemea kinachobaki ndiyo ujilipe,hutabaki na chochote na hutaweza kuweka akiba.

Kanuni hiyo pia inafanya kwenye eneo la muda. Kama unatumia muda wako kwa yale yanayokuja mbele yako ukijiambia baada ya kukamilisha hayo utapata muda wa kufanya yaliyo muhimu unajidanganya,haitakuwa kutokea umalizie kila kitu na ubaki na muda.

Badala yake unapaswa kujitengea muda wako kwanza,wa kufanya yale muhimu zaidi kwako, bila kujali una mengine mengi kiasi gani ya kufanya.

Hapa unatenga saa moja mpaka mawili kila siku kwa ajili yako mwenyewe ambayo unatumia muda huo kwa yale muhimu zaidi kwako.

Haijalishi nini kinaendelea kwenye maisha yako,huachi kutenga muda huo muhimu kwa ajili yako. Kwa kufanya hivi,moja kwa moja yale yasiyo muhimu sana yatakosa muda kwenye maisha yako na hapo unakuwa mghairishaji mzuri.

Msingi wa pili ni kuweka ukomo kwenye mambo unayofanyia kazi kwa wakati mmoja. Wengi huwa wana mambo mengi wanayofanyia kazi kwa wakati mmoja,wakiona hiyo ni njia nzuri ya kukamilisha mambo mengi kwa wakati mmoja .

Lakini kinachotokea ni wanashindwa kukamilisha chochote kikubwa kwenye maisha yao. Kama kila wakati unakubali kupokea na kuanzisha kitu kipya unaishia kuzitawanya sana nguvu zako na hakuna kikubwa utakachoweza kukikamilisha.

Unapaswa kuchagua kufanyia kazi mambo makubwa machache kwa wakati mmoja,yasizidi mambo matatu . Yaani katika wakati wowote wa maisha yako,unapaswa kuwa na mambo makubwa yasiyozidi matatu unayofanyia kazi.

Msingi wa tatu ni kuheshimu vipaumbele vyako na kuachana kabisa na yale ambayo siyo kipaumbele kwako. Ukishajiwekea vipaumbele,kuna mambo yatakuwa kwako ambayo unaweza kuyaona ni mazuri na yanayofaa.

Lakini kama hayajaingia kwenye vipaumbele vyako,jua huo ni mtego wa kukuondoa kwenye vipaumbele. Yakatae kabisa mambo yote mazuri unayoshawishika kufanya kama hayapo kwenye vipaumbele vyako.

Kusema hapana ni hitaji muhimu sana hapa. Na ugumu wa kusema hapana unakuja pale ambapo unachopaswa kukisemea hapana na kitu unachopenda kufanya .

Kuchukua hatua, rafiki yangu tunapaswa kuelewa kwamba kama tunataka kufanya makubwa, hatuna budi kusema hapana kwenye mambo mazuri tunayovutiwa kuyafanya ila hayapo kwenye vipaumbele vyako.

Akupendaye sana.

Mwandishi Maureen Kemei,

Mawasiliano:

kemeimaureen7@gmail.com.

www.uamshobinafsi.com

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *