Umuhimu wa kubadili mtazamo wako.

Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini kuna hadithi maarufu kutoka katika kitabu cha Acres of diamonds cha Russell H. Conwell, kinachomhusu mkulima aliyeuza shamba lake baada ya mtu mwenye hekima kumwambia kuwa akiwa na kipande kidogo cha almasi kama kidole gumba chake anaweza kuwa tajiri mkubwa na mwenye nguvu, pia akiwa na kipande cha almasi kama tofali anaweza akamiliki nchi yote.

Mkulima yule ajulikanaye kwa jina la Faitz, usiku ule hakulala kabisa na alikuwa hana furaha kabisa usiku kucha. Kesho lake alifanya mambo ya kuuza shamba lake, aliamua kuuza shamba lake lote na kwenda kutafuta almasi.

Alizunguka Africa yote lakini hakuweza kuiona, akazunguka Ulaya nzima lakini hakuiona, hatimaye alipofika Uhispania akiwa amechoka na hela zimemwishia, aliamua kujiua kwa kujitosa kwenye Mto Barcelona.

Huku nyuma aliyenunua shamba la mkulima, siku moja alikuwa ananywesha maji ngamia katika kijito cha maji kilichokatiza katika shamba lile. Miale ya jua iliangazia jiwe lililokuwa karibu na kijito kile, na lilitoa rangi ya kumetameta kama rangi ya upinde wa mvua. Yule jamaa mwenye shamba alilichukua lile jiwe na kuliweka ndani yake.

Yule mwenye hekima alipokuja na kuliona lile jiwe aliuliza swali Faitz amekuja? Faitz ndilo lilikuwa jina la yule mtu aliyeuza shamba. “Hapana,” yule aliyekuwa amelinunua shamba alijibu na akamuuliza ” Kwa nini anauliza hivyo?” “Kwa sababu ile ni almasi.”

Yule mmiliki mpya wa shamba alisema ” Hapana, ni jiwe tu ambalo nimeliokota kwenye kijito na yapo mengi tu.” Walienda kuokota na kwenda kuyafanyia uchunguzi na kweli walikuta yale mawe ni almasi. Katika shamba lile kulikuwa na heka za almasi.

Mambo muhimu ya kujifunza kutokana na hadithi hii, kutoka katika kitabu cha Acres of diamonds cha Russell H. Conwell.

Kwanza kama mtazamo yetu iko sahihi au ni chanya tunapaswa kugundua kuwa wote tunatembea kwenye heka za almasi. Hakuna aliye masikini bali ni kutojua siri hii. Kwani kila mtu anao uwezo ndani yake wa kumwezesha kutimiza kusudi lake la kuwa hapa dunia.

Kuchukua hatua, rafiki yangu uwezo wa kutimiza ndoto yako upo mikononi mwako. Unaweza kufikia malengo na kutimiza ndoto yako kama ukitambua kuwa unao uwezo katika ncha za vidole vyako.

Hii inahitaji uwe na mtazamo chanya. Fursa mara nyingi huwa ziko chini ya miguu yetu. Wala haihitaji kwenda mbali, kinachohitajika ni kutambua tu hizo fursa.

Dkt. Eli VD Waminiani aliwahi kusema, ” Watu wengi ni masikini kwa sababu wanahangaika kutafuta utajiri mbali na mahali walipo, lakini kumbe utajiri wanaona mikononi mwako” Watu wengi hawafanikiwi kwa sababu wanahangaika kutafuta vitu ambavyo tayari wanavyo.

Ukitafuta kitu ambacho unacho hutakipata, bali unatakiwa kukitambua na kukitumia ili kukinufaishe.

Akupendaye sana,

Maureen Kemei.

kemeimaureen7@gmail.com

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *