Ni nini adui wa mafanikio yako?

Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini kila kitu kizuri chenye manufaa huwa kinakuwa na maadui wake.

Kadhalika ufanisi wa hali ya juu huwa unakuwa na maadui ambao unapaswa kuwajua na kuwashinda ili uweze kujijengea hali hizo mara kwa mara na kufanya makubwa.

Adui wa kwanza ni kufanya mambo mengi kwa pamoja. Huwezi kuzama kwenye ufanisi wa juu kama akili yako inahangaika na mambo mengi kwa wakati mmoja. Chagua kufanya jambo moja tu kwa wakati na achana na mengine yote katika wakati huo.

Adui wa pili ni msongo. Msongo wa mawazo huwa unaondoa umakini wa mtu kwenye kile anachofanya na kuupeleka kwenye mambo mengine yanayomsumbua.

Kabiliana na yale maeneo ya maisha yako yanayokupa sana msongo, iwe ni kazi, mahusiano au afya, tatua vyanzo vyote vya msongo.

Na pia unapopanga kufanya kitu ambacho unataka kuzama kwenye ufanisi wa juu, sahau yote yanayokupa msongo katika wakati huo. Jiambie unajipa muda mfupi wa kusahau yote yanayokusumbua na kuweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya.

Adui wa tatu ni hofu ya kushindwa. Kutaka ukamilishaji ni kikwazo kikubwa kufika kwenye ufanisi wa juu. Kama unataka kufanya kwa ukamilifu mkubwa, kama unaona kukosea au kushindwa ni fedheha kubwa, umakini wako utaenda zaidi kwenye hofu ya kushindwa kuliko kufanya kitu husika.

Sahahu kuhusu ukamilishaji, acha kufikiria kushindwa. Wewe fikiria kile tu unachofanya na hapo utaweza kuzama kwenye ufanisi wa juu.

Adui wa nne ni kutokuamini kile unachokifanya. Kama huamini kweli kwenye kile unachofanya, kama hujiamini kwamba unaweza kukifanya, hutaweza kuzama kwenye ufanisi wa juu.

Amini kwenye kile unachofanya kwamba ni muhimu, na kinawezekana. Jiamini kwamba una uwezo wa kukifanya, ujuzi na maarifa yote muhimu. Kwa kuwa na Imani hivyo, utaweza kuzama kwenye ufanisi wa juu na kufafanua makubwa.

Kuchukua hatua Ili uweze kufanya makubwa na kuondoa kila aina ya ukomo kwenye maisha yako, jijengee hali hizo za ufanisi wa juu kwenye yale makubwa unayofanya.

Akupendaye sana,

Maureen Kemei.

kemeimaureen7@gmail.com

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *