Rafiki yangu mpendwa watu wote wenye ufanisi mkubwa na ambao wanafikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao ni watu makini.
Ni watu ambao wana maono kwenye maisha yao na wanayaishi maono hayo. Watu hawa wanajua ni nini wanachotaka kwenye maisha, na wanakifanya kazi kila siku.
Watu wenye ufanisi mkubwa wanajua ya kwamba maisha yao ni jukumu lako na hivyo wanachukua hatua katika kuyafanya yawe bora. Hawalalamiki wala kulaumu wengine, badala yake kama kuna kitu hakipo sawa wanachukua hatua.
Lakini wale wanaokosa ufanisi mara zote huangalia ni nini wamekosa na kuanza kutafuta watu wa kulaumu au kulalamika.
Mtu mwenyewe ndiye mwenye mamlaka ya mwisho juu ya maisha yao, haijalishi ni kitu gani kimetokea, maamuzi ya mtu ndiyo yanayopelekea kufaidika au kutofaidika.
Hata kama mtu amekutukana, siyo tusi ambalo litakuumiza wewe, bali iwe maana ya tusi unavyoichukulia. Watu wenye ufanisi hawaruhusu hali za nje kuwavuruga, wasiokuwa na ufanisi huvurugwa na kila kinachotokea kwenye mazingira yao.
Watu wenye ufanisi mkubwa wanajua matatizo yote tunayokutana nayo kwenye maisha yetu kwenye makundi matatu;
- Matatizo ambayo yanatuhusu sisi moja kwa moja, ambayo yanatokana na tabia zetu au matendo yetu, haya wanayafanyia kazi mara moja.
- Kundi la pili ni matatizo ambayo hayatuhusu moja kwa moja, ambayo yanatokana na matendo ya wengine; haya huyashughulikia kwa kubadili mtazamo wao.
- Kundi la tatu ni matatizo ambayo yako nje ya uwezo wetu, ambayo hatuwezi kufanya chochote, haya wanaachana nayo. Wasio na ufanisi wanachanganywa na kila tatizo.
Kuchukua hatua; rafiki yangu amua kuchukua hatamu ya maisha yako, amua kupanga ni jinsi gani maisha yako unataka yaende.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.