Njia 4 za kubadili mtazamo kuhusu fedha na utajiri.

Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini fedha na utajiri ni kitu ambacho kimekuwa kinawachanganya wengi.

Kila mtu anataka kupata fedha na utajiri na kuweka kila juhudi ili kupata. Lakini ni wachache pekee wanofanikiwa kupata fedha na utajiri.

Kinachowatofautisha wanaopata na wanaokosa siyo juhudi wanazoweka, bali mtazamo wanaokuwa nao.

Kuna mtazamo ya aina nne ambayo unapaswa kuibadili Ili kupata fedha na utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

Moja ni uhaba. Wengi wanachukulia fedha kwa uhaba, kwa kuona njia pekee ya kuzipata ni kuzikumbatia na kuzificha. Mtazamo huo unaifanya asili ione mtu hayupo tayari kupata zaidi na hivyo kumfanya asione fursa za kupata zaidi.

Ondokana na mtazamo wa uhaba na jijengee mtazamo wa utele. Ona fedha ziko tele na unaweza kupata nyingi uwezavyo. Hivyo huna haja ya kuficha au kukumbatia fedha ulizonazo, badala yake unapaswa kuzizungusha ili zizalishe zaidi na zaidi.

Mbili ni kufa na kupona. Wengi huchukulia fedha kama kitu cha kufa na kupona, kwamba kama wakizikosa basi ndiyo maisha yamefika mwisho.

Hii inawafanya waishi kwa hofu kubwa na hofu hiyo inawazuia wasione fursa nzuri za kupata fedha zaidi.

Ondoa mtazamo huo wa kufa kupona na jenga mtazamo wa fedha kuwa kama mchezo. Kwamba kupoteza mchezo mmoja sio kama kushindwa, kuna michezo mingi mbeleni.

Kukosa au kupoteza fedha haimaanishi ndiyo mwisho wa maisha yako, bali ni sehemu ya maisha, unapokuwa na utulivu na kufanya yaliyo sahihi, utapata fedha zaidi.

Tatu ni ushindani. Wengi Wana mtazamo wa ushindani, kwamba ili wao wapate lazima wengine wakose. Wanaishi kwa ulimwengu wa pata potea au jumla sifuri.

Wanaamini ili wao wapate lazima wengine wakose. Huo ni mtazamo ambao unawazuia watu wasione fursa nzuri za kutoa thamani zaidi na kupata fedha zaidi.

Rafiki yangu ondokana na mtazamo huo na jenga mtazamo wa ushirikiano, jua unaweza kupata fedha kwa kuwawezesha wengine kupata fedha pia.

Kwa kuongeza thamani kwa wengine, matokeo yanakuwa ni jumla chanya, wewe unapata na wengine pia wanapata. Kwa mtazamo huu, utaziona na kuzitumia fursa zaidi za kuongoza kipato chako.

Nne ni kuchukua. Wengi wana mtazamo wa kuchukua au kupewa zaidi kuliko wanavyotoa . Kwa chochote wanachofanya, wanajiangalia kwanza wao wananufaikaje na hawajali wanawanufaishaje wengine. Ndiyo maana watu wanakuwa tayari kushiriki kwenye rushwa na ufisadi, kwa sababu wanataka kupata zaidi ya wengine.

Lakini mtazamo huu huwa kikwazo kwao kupata zaidi na zaidi. Badili mtazamo huo na jenga mtazamo wa kutoa, mtazamo wa kujali maslahi ya wengine badala ya kujali maslahi yako tu.

Hatua ya kuchukua; Kwa kuangalia unawanufaishaje wengine, unaweza kutoa manufaa makubwa zaidi tu ambacho kitafanya ulipwe zaidi.

Akupendaye sana,

Maureen Kemei.

kemeimaureen7@gmail.com.

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *