Jinsi ya kuwa paka kwenye zama hizi.

Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini Mwandishi Jaron katika kitabu chake cha Ten Arguments for Deleting Your Social Media Accounts Right Now, anatushirikisha mfano ya wanyama wawili ambao binadamu tunaishi nao, anasema wanyama hao ni paka na mbwa.

Anasema mbwa walianza kuishi na binadamu kwa sisi binadamu kuwakamata nakuwafuga, hivyo mbwa wamekuwa wakimsikiliza na kumtii binadamu. Mbwa wamebadilishwa tabia na binadamu kufundishwa kuwa watiifu.

Lakini paka ni tofauti, paka hakukamatwa na kufungwa na binadamu, paka walikuwa wenyewe na kuanza kuishi na binadamu. Hivyo paka wana uhuru mkubwa kuliko mbwa. Ndiyo maana unaweza kuswaga kundi la mbwa, lakini siyo kundi la paka.

Paka hajawahi kubadilishwa tabia zake na binadamu, paka anaishi maisha yake kwa uhuru, huwa hafuati hata kundi. Na ndiyo maana tunawapenda sana paka, japo hawana matumizi makubwa kwetu kama kwa mbwa ambao tunawatumia kwa ulinzi.

Mwandishi anaendelea kuelezea kwamba katika mabadiliko yote yaliyotokea duniani, viumbe wengi wamebadilika isipokuwa paka. Paka hajawahi kukubali kutawaliwa na yeyote, wako huru kuyaishi maisha yao na kufanya maamuzi yao.

Japokuwa tunawapenda mbwa, hakuna anayependa kuwa na tabia kama za mbwa, za kubadilishwa kitabia na kuwa mtiifu kwa wengine. Kila mtu anataka kuwa huru kufanya maamuzi yake mwenyewe, lakini mitandao ya kijamii imekuja kuwa hatari kwetu.

Mitandao hiyo kwa njia mbalimbali imekuwa inatubadili tabia kama ambavyo mbwa wanafundishwa utiifu.

Kitu kimoja zaidi rafiki ni kuwa wapo watu wanatumia mitandao hiyo ya kijamii kutusukuma kufanya vitu fulani bila ya sisi kujua kama tumesukumwa kufanya hivyo.

Mwandishi anatuambia lengo la kitabu chake ni kutufundisha jinsi ya kuwa paka, kupaki na uhuru wa kufanya maamuzi yetu wenyewe kwenye dunia ambayo mitandao ya kijamii imetawala maisha ya watu na kuwashawishi kufanya vitu visivyo na manufaa kwao.

Mwandishi anasema kuwa mitandao ya kijamii inatuhadaa kwamba hakuna maisha nje ya mitandao hiyo, lakini huo siyo ukweli, ni njia ya kuifanya iendelee kujinufaisha huku ikivuruga maisha yako.

Kuchukua hatua; rafiki yangu tunahitajika kuwa paka kwenye nyakati hizi, yaani kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yetu wenyewe na hivyo kuwa huru.

Rafiki yako,

Maureen Kemei.

kemeimaureen7@gmail.com.

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *