Umuhimu Wa Wewe Kuwa Tajiri.

Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini kinachowatofautisha wanaotajirika na wanaobaki masikini ni tabia.

Hivyo kwa kuzijua tabia za kitajiri na kuziishi kwenye maisha yako ya kila siku, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufikia utajiri pia.

Mambo mengi sana yamekuwa yanasemwa kuhusu utajiri na matajiri, lakini mengi kati ya mambo hayo siyo sahihi. Mengi yanasemwa kuhusu utajiri na matajiri, hasa kwa upande hasi siyo sahihi na yamewafanya wengi kuendelea kubaki kwenye umasikini.

Ukweli ni kwamba utajiri ni mzuri, pale mtu unapoweza kuwa na fedha unazohitaji kwa ajili ya mahitaji ya maisha yako. Na pale unapokosa fedha, maisha yanakuwa siyo bora, kuanzia kwako binafsi na hata kwenye mahusiano yako.

Hivyo yeyote anayesema utajiri siyo muhimu, anajidanganya tu na kujipa moyo. Fedha na utajiri ni vitu muhimu sana kwenye maisha yetu ya kila siku.

Ukweli wa kuumiza ni kwamba katika kila jamii, yaani ukianza na dunia nzima, ukaja kwenye nchi ukaenda kwenye mkoa, wilaya na hata mtaa, utajiri umegawanyika kwenye namba ambazo ni sawa kwenye kila eneo. Namba hizo ni 99/1,95/5 na 90/10.

Namba ya kwanza ni 99 kwa 1, ikimaanisha asilimia 1 ya watu kwenye eneo ndiyo wenye utajiri mkubwa mno duniani, kushinda asilimia 99 kwa ujumla. Hii ina maana katika watu 100, mmoja ana utajiri mkubwa kushinda jumla ya utajiri wa wale wengine tisini na tisa.

Namba ya pili ni 95/5 ikimaanisha asilimia 5 ya watu kwenye eneo ndiyo wanaokuwa na utajiri na uhuru wa kifedha, huku asilimia 95 wakiwa na maisha ya kawaida au ya chini kabisa. Wale waliopo kwenye asilimia 5 hata kama siyo matajiri kama asilimia moja, lakini maisha yao yana ya uhuru mkubwa. Hawa hutawaona kwenye orodha ya matajiri wakubwa, lakini wameshafikia uhuru wa kifedha na wanaishi maisha bora sana kwao.

Namba ya tatu ni 90 kwa 10, ambapo asilimia 10 ya watu wanakuwa na utajiri au maisha ya juu, huku asilimia 90 ya watu wakiwa na maisha magumu sana. Hii ina maana katika watu 100, watu 90 wapo kwenye hali ngumu sana kifedha, hawana uhakika kesho au mwezi ujao wanaendeshaje maisha yao. Hawa ni watu ambao kila wakati wanaishi kwa wasiwasi kwa sababu hawana msingi wowote kifedha.

Namba sahihi kwa wewe kuwa ni kwenye 95/5 unapaswa kuwa kwenye asilimia 5 ya juu kwenye jamii yako na hata dunia kwa ujumla kwa kuwa na uhuru wa kifedha, kuwa na fedha ambazo unaweza kuendesha maisha yako kwa namna unavyotaka wewe.

Hii ni namba sahihi kwako kwa sababu hujitaji kushindana na yeyote na wala hujitaji kuwa na bahati kuifikia. Kwa kujijengea tabia nzuri, kuweka juhudi kubwa na kutokukata tamaa, utaweza kufika kwenye asilimia 5 ya juu na maisha yako yakawa bora sana.

Kabla hujafanya maamuzi napenda kukushirikisha kauli ambayo Kocha Dr Amani Makirita huwa anasema kuwa, utajiri ni mchezo, mchezo ambao una kanuni zake na sheria zake. Na ili uweze kushinda mchezo huu, lazima uzijue kanuni na uzishike sheria.

Wengi wamekuwa wanaingia kwenye mchezo wa utajiri kama vile ni kitu cha kubahatisha, hawajui kanuni wala sheria, hawana maandalizi na kinachotokea ni kushindwa vibaya sana.

Kuchukua hatua, rafiki yangu tuna kazi kubwa ya kufanya, kuhakikisha kuwa tunapambana ili tuifikie namba sahihi ya utajiri ya 95/5. Kwa sababu tunakuwa tunajijengea tabia nzuri ya kuweka juhudi kubwa kwenye kazi na biashara zetu, na pia kuweza kuwekeza kwa namna sahihi bila kukata tamaa. Na bila shaka tutafikia utajiri na uhuru wa kifedha na kuweza kufanya mambo yetu kwenye maisha yetu.

Rafiki yako,

Maureen Kemei.

kemeimaureen7@gmail.com.

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *