Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini kwa chochote ambacho mtu unafanya, unapaswa kuwa na lengo halisi linalokuongoza.
Unapokosa lengo, unajikuta ukihangaika na kila kitu, maana kila kitu kinakuwa na umuhimu kwako.
Seneca anashauri hata kwenye usomaji wa vitabu, bila malengo mtu anajikuta anahangaika na kila kitabu, akisoma vingi kwa haraka na asiwe na uelewa wowote.
Kwa Seneca lengo sio umesoma vitabu vingapi, bali lengo ni nini umeelewa kupitia usomaji wa vitabu.
Pamoja na kusisitiza mtu kuwa na lengo ambalo anafanyia kazi, Seneca pia hajasahau umuhimu wa mapumziko na starehe.
Kwa Seneca kufanya kazi muda wote bila mapumziko na starehe ni kujinyima furaha kwenye maisha.
Seneca alikwenda mbali mpaka kuandika kitabu alichokiita on leisure, akielezea umuhimu wa mapumziko na starehe kama sehemu ya kutuliza akili na mwili.
Utulivu huo ni muhimu kwa furaha na kupata msukumo wa kuendelea kufanyia kazi malengo.
Seneca pia aliamini furaha yako haitegemei mazingira ya nje, bali hali ya ndani ya mtu . Alieleza unaweza kuwa na furaha ukiwa popote, kama tu hali yako ya ndani iko vizuri.
Anasema amewahi kuona watu walio ndani ya mahekalu yenye kila kitu ila hawana furaha. Na pia amewahi kuona watu wakiwa peke yao kwenye mazingira magumu ila wana furaha kubwa .
Hivyo kama huna furaha, kabla hujakimbilia kubadili mazingira ya nje, jichunguze kwanza ndani yako.
Chukua hatua, kama ndani hakujakaa sawa, hata ukibadili mazingira, utaishia kuwa vilevile.
Kitu kimoja zaidi, tunapaswa kuhakikisha ndani yetu kuna furaha ili tuweze kuleta mabadiliko hata na mazingira yetu.
Mwandishi wako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.