Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini changamoto kubwa kabisa kwenye hofu ni pale tunaposhindwa kuielewa kwa undani. Unapoiona hofu kwa nje inakuwa inatisha sana.
Usipoichambua hofu kwa undani, hutaweza kuchukua hatua, maana utaiona ni kikwazo kikubwa.
Kwa kila hofu unayokuwa nayo, usiishie tu kuiangalia kwa nje, bali ichimbe kwa undani, uweze kuielewa na kuchukua hatua sahihi.
Hatua muhimu ya kuchukua ni kujiuliza kipi kibaya zaidi kinachoweza kutokea?
Kwa chochote unachohofia, usikubali tu hofu hiyo juu juu. Badala yake chimba ndani, jiulize kipi kibaya zaidi kinachoweza kutokea kwenye hilo unalohofia.
Jiulize kama kweli hofu hiyo itatokea kama unavyohofia, ni mambo gani mabaya kabisa yanayoweza kutokea?
Orodhesha yote mabaya unayoona yanaweza kutokea kutokana na kile unachohofia. Kisha kwa kila unaloorodhesha jiulize ni hatua zipi unazoweza kuchukua kulikabili kama litatokea.
Andika hatua zote unazokwenda kuchukua pale jambo baya kabisa linapotokea ili uweze kurudi kwenye mipango yako.
Kwa kufanya zoezi hili, unagundua wazi kwamba mengi unayohofia hayawezi kutokea na hata kama yatatokea una njia ya kuweza kuyavuka na kuendelea na mipango yako.
Chukua mfano wa kuanzisha biashara, hofu ni itashindwa. Kibaya zaidi kinachoweza kutokea ni biashara kufa na ukapoteza kila kitu.
Kama hilo litatokea unaweza kuanza upya, hata kwa kutafuta kazi au kibarua kwanza ili ujenge upya.
Chukua hatua kwa kuchambua hofu hivi, unaona wazi kwamba unachohofia sana hakipaswi kuwa kikwazo kwako.
Mwandishi wako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.