Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini pale unapofanya kitu chochote cha tofauti na cha kibunifu, moja kwa moja unakuwa umekaribisha wakosoaji.
Rafiki yangu, nadhani bado hujaweza kuelewa kuwa kukosolewa ni sehemu ya maisha ya kila siku.
Yaani kila siku kuna watu wanakukosoa kwa namna mbalimbali. Unavyovaa, unavyofanya kazi zako, unavyoishi maisha yako.
Watu unaokutana nao njiani na wasiokujua kwa namna yoyote ile wanakuhukumu. Watu wako wa karibu pia wanakuhukumu. Watu unaokutana nao mitandaoni wasiojua chochote kuhusu wewe pia wanakuhukumu.
Hata wewe mwenyewe kuna wakati huwa unajihukumu kwa yale unayofanya. Na pia umekuwa unawahukumu watu wengine hata usiowajua kwa undani. Kuhukumu ni sehemu ya maisha ya wanadamu.
Hivyo usiumie pale unapohukumiwa au kukosolewa, badala yake jua upo ukosoaji mzuri kwenye manufaa kwako na upi siyo mzuri unaopaswa kuupuuza.
Tambua kila kitu unachokipenda na kukikubali kwenye maisha, kuna wengine ambao hawakupendi hawakukubali.
Kuwepo kwa watu wanaochukia kile unachopata haimaanishi ni kitu kibaya, bali ni wao hawawezi kukielewa.
Kile ambacho wengi wanasema ni ukosoaji, siyo ukosoaji kweli, bali ni maoni yao kuhusu kitu fulani.
Tatizo la maoni kila mtu ana yake na huwa yanachochewa zaidi na hisia hivyo hayawi sahihi.
Mtu anapokosoa kitu kwa sababu hakipendi au hakielewi, ukosoaji wake hauwezi kuwa sahihi, hayo ni maoni yake, ambayo siyo ukweli.
Chukua hatua; tambua kwamba chochote unachofanya siyo kwa ajili ya kila mtu, bali kwa ajili ya watu wa aina fulani ambao unajua jinsi ya kuwafikia.
Unapochagua wale unaowalenga, unawaandalia kile chenye manufaa kwao na kuwapuuza wengine.
Watu hao wanapokupa maoni yao, yanakuwa na manufaa kwako kwa sababu yanaendana na kile unachofanya.
Mwandishi wako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.