Rafiki yangu mpendwa huwa tunakatishwa tamaa kutokana na kuwaambia watu ndoto zetu ambao hawafanani na sisi kimaono na hata kimtazamo kabisa.
Kwa mfano ukienda kuomba mtu ushauri mtu aliyekata tamaa ya maisha sidhani kama utapata tumaini la maisha kutoka kwake.
Kuna watu ukienda kuongea nao unajihisi tayari wewe ni mwanamafanikio lakini kama kuna wengine ukiongea nao wanakutoa katika hamasa ya mafanikio kabisa.
Nani unayemwambia ndoto zako? Mtu hasi au chanya? Kumwambia mtu hasi ndoto zako ni mwanzo wa kujichimbia kaburi wakati bado uko mzima.
Huwa tunakuwa na ndoto kubwa kweli, tunapenda kufanya mambo makubwa na tunakuwa na hamasa lakini tunawaambia watu ambao siyo sahihi katika ndoto zetu huwa tunajiharibia wenyewe.
Watu hasi huwa wanazima ndoto za watu wengi kama vile mshumaa unavyopotea .
Rafiki, kama umekosa watu chanya wa kuambatana nao katika jamii yako, wako marafiki chanya siku hizi unaweza kutembea nao ambao ni kama vile vitabu, watu chanya waliofanikiwa, kuliko kupoteza muda na watu hasi tumia muda wako kusoma vitabu utakuwa chanya.
Haijalishi watu wanasema nini, lakini wewe ndiyo unatakiwa kuwa chanya zaidi ya wengine wote katika kile unachoamini.
Wewe ndiyo dereva wa maisha yako unajua wapi unataka kwenda usikubali mtu aje akurudishe nyuma na kukupitisha njia ambayo siyo kabisa. Una maamuzi ya kuamua vile unavyotaka usiwaruhusu watu wakuamulie sana maisha yako wakati wewe mwenyewe bado uko hai.
Ukiwa umekufa basi unakuwa huna thamani na huna kauli ya kusema ufanyiwe vipi na maiti haina haki. Sasa wewe uko hai kubali kutetea haki zako usikubali uwe maiti wakati uko hai.
Hatua ya kuchukua, uwe na msimamo mkali juu ya maisha yako. Watu wakujue kabisa wewe ni mtu wa namna gani.
Usiwe ni mtu wa ndiyo kwa kila mtu badala yake kuwa mtu wa hapana na ukiamua kufanya kitu fanya kweli na washangazwe watu kwa matokeo bora. Chochote kinachopita kwenye mkono wako acha alama isiyofutika.
Mwandishi,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.