Rafiki yangu mpendwa, jamii huwa inapenda tuwe wa kawaida ili iwe rahisi kutudhibiti. Hivyo pale unapoenda tofauti na jamii inavyotaka uwe, unaonekana kama mtu wa ajabu na aliyepotea. Lakini hiyo ndiyo njia pekee ya kufanya makubwa na kufanikiwa.
Huwezi kufanikiwa kwa kufanya yale yaliyozoeleka na kuwa kama wengine wanavyotaka uwe. Utafanikiwa kwa kujisikiliza mwenyewe, kutambua utofauti wako na kuuishi. Usijiskie vibaya pale unapokuwa tofauti na wengine. Jua huo utofauti wako utakaokufikisha kwenye mafanikio makubwa, kama utaweza kuutumia vizuri.
Unapoujua utofauti wako usiufiche wala kujionea aibu, badala yake uishi kwa kujivunia. Hata kama watu hawakuelewi, wewe ishi huo utofauti wako na waache wayaone matokeo ya tofauti unayozalisha kupitia utofauti wako.
Jamii inapenda kuwaweka watu kwenye makundi ya kazi ambayo yanaeleweka . Hivyo itakulazimisha pia ujitambulishe kwa kundi fulani linaloeleweka. Kama wewe unaona hakuna kundi moja linalokufaa, usijilazimishe kuingia kwenye kundi lolote. Wewe tengeneza kundi lako linalokufaa, linaloendana na utofauti wako.
Jamii inapenda kuwaambia watu wabobee kwenye kitu kimoja. Kama hilo lipo ndani yako fanya hivyo. Lakini ndani yako unasukumwa kufanya kitu zaidi ya kimoja, fanya. Muhimu ni kutokuzima moto mkubwa unaowaka ndani yako, kwani huo una nguvu ya kukuwezesha kufanya makubwa.
Ukweli ni hakuna mtu yeyote anayekujua wewe na uwezo mkubwa ulio ndani yako. Wakati mwingine hata wewe mwenyewe hujijui vizuri, kwa sababu umekuwa unahangaika na mengi na kujisahau wewe mwenyewe.
Chukua hatua, rafiki yafanye maisha yako kuwa safari ya kujitambua, kujisikiliza na kupambana kuwa bora kadiri unayokwenda. Kwa kufanya hivyo, utaweza kufanya makubwa na ya tofauti kabisa na yale wanayofanya wengine.
Mwandishi wako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com