Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini kufikiri kwa usahihi na umakini ni muhimu kuliko kuwa na akili.
Wapo watu wengi wenye akili sana ila hawana hekima na hivyo hawafanyi maamuzi sahihi.
Wewe unapaswa kujijengea uwezo wa kufikiri kwa usahihi na umakini, kwa kujua msingi wa kitu na kujua jinsi kinaungana na vitu vingine na unapofanya maamuzi, unajua kabisa ni matokeo gani yanakwenda kupatikana.
Ili kufikiri kwa usahihi unahitaji vitu viwili; Kitu cha kwanza ni kuepuka kuathiriwa na hisia zako wakati wa kufikiri na kufanya maamuzi. Hisia zinapokuwa juu, huwezi kufikiri kwa usahihi. Hivyo kuwa na njia ya kutuliza hisia zako au kuwa na subira mpaka zinapotulia ndipo ufikiri na kufanya maamuzi.
Kitu cha pili ni kujua misingi ya kitu kabla hujafanya maamuzi. Kila kitu kina msingi yake ambayo huwa haibadiliki, ukijua msingi hiyo inakusaidia sana kufanya maamuzi ambayo ni sahihi.
Utajua kama unafikiria kwa usahihi kuhusu kitu kama unaweza kumwelezea mtoto wa darasa la tano na akakuelewa au mzee ambaye hakuenda shule kabisa.
Kama chochote unachofanya huwezi kukielezea kwa namna sahihi kwa mtoto wa darasa la tano kuelewa, basi wewe mwenyewe hujui unachofanya na huwezi kufanya maamuzi sahihi kwenye eneo hilo.
Kwenye kila tasnia, kuna mambo mengi na mengi zaidi yanagunduliwa kila siku. Huwezi kupata muda wa kuweza kujifunza na kujua kila kitu, ila yale ya msingi huwa ni machache na hayabadiliki. Ukiyajua hayo ya msingi, utaweza kufanya maamuzi bora na sahihi kwenye eneo hilo.
Kuchukua hatua; rafiki yangu tunapaswa kuepuka sana kutumia lugha na dhana ngumu kwa wengine kuelewa Ili tuonekane kama tunajua, badala yake tunapaswa tukijue kitu kwa misingi yake, kwa namna ambayo tunaweza kumweleza yeyote na akaelewa, hapo tunakuwa tumekielewa vizuri na kuweza kufanya maamuzi sahihi.
Mwandishi wako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.