Rafiki yangu mpendwa nianze kwa kusema, usinunue matatizo ya wengine. Rafiki matatizo uliyonayo, tayari yanakutosha hivyo usinunue mengine.
Muda uliokuwa nao kufanya vitu vya msingi ni mdogo mno. Ukisema uhangaike na kila kitu kwenye hii dunia basi utakufa haraka.
Ukisema uhangaike na matatizo ya kila mtu hutaweza kuyamaliza. Kwanza matatizo ya watu, huwa yanamalizwa na watu wenyewe. Unaweza kuwa mtu wa huruma sana kusikiliza matatizo ya watu na kutaka kuwasaidia lakini matatizo ya watu huwa yanamalizwa na watu wenyewe.
Matatizo ya watu ni mengi, na wengine wanapenda kuwauzia watu wengine matatizo yao. Hivyo, usipokuwa makini, utajikuta kila siku unasikiliza drama za watu.
Na watu ni waigizaji sana, usipokuwa makini, watakuigizia na kuja kuona kwamba jukumu la maisha yao ni lako.
Watu wengi hawajui kwamba, jukumu la maisha yao, ni la kwao wenyewe. Wafanye watu unaohusiana nao, wajitambue na wajue kwamba jukumu la maisha yao ni lao mwenyewe.
Watu wengi ambao wameanza kupata mafanikio kidogo kwenye jamii zetu, wamekuwa wanapata shida sana, kila mtu anamuona kama ndiyo kimbilio la maisha yake, watu hawajitumi na wanajua nikiwa na shida nitasaidiwa na fulani.Na usipokuwa makini, utakuwa unanufaika matatizo yao kila siku na kushindwa kufanya mambo yako.
Kila mtu afanye kazi na afundishwe kujitegemea na kusimama na mambo yake. Usiruhusu utegemezi ambao hauna maana kwako, na usikubali kununua matatizo ya watu.
Watu wengine wanatengeneza matatizo ili uweze na wewe kuingia kwenye matatizo hayo.
Hatua ya kuchukua leo; kuwa mkali kwa watu wako wa karibu ambao wanashindwa kujitegemea na kufanya utegemezi kwako.
Wafundishe kujitegemea na kutambua kuwa jukumu la maisha yao, ni lao wenyewe.
Kama mtu ana nguvu, anaweza kufanya kazi, afanye kazi ili maisha yake yaende na siyo kukubali kusaidia majukumu binafsi ya watu ambao wana uwezo wa kufanya kazi.
Watu wana uvivu, uzembe wa kutokufanya kazi. Wanapenda kupata mteremko, usikubali kuwaonesha hilo, wasaidie wasimame na miguu yao na kutambua kuwa jukumu la maisha yao ni lao na siyo lako.
Mwandishi wako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.