Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini hakuna kitu kinatuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu kama maamuzi ya kukurupuka.
Unakuwa unafanya maamuzi bila ya kufikiri kwa kina na mwishowe yanakuwa na madhara makubwa kwako. Wakati unafanya maamuzi hayo unaona kila kitu kipo sawa, lakini unapokuja kukaa chini na kufikiri kwa kina, unaona namna ulifanya maamuzi bila ya kuwa na taarifa sahihi.
Hii ni tabia ambayo unahitaji kuivunja haraka sana kama unataka kufanikiwa na kudumu kwenye mafanikio. Na jinsi ya kuivunja tabia hii ni kuzingatia yafuatayo;
Kwanza; jiridhishe na taarifa kabla hujafanya maamuzi. Kabla hujafanya maamuzi yoyote makubwa na muhimu, jiridhishe na taarifa unazopata. Je ni taarifa za kweli, je ni taarifa sahihi, je ni taarifa za kutosha. Mara nyingi watu wanaweza kuwa na taarifa ambazo siyo za kweli, au taarifa za kweli lakini hazijajitosheleza, wanatumia kufanya maamuzi na wanaumia. Chunguza taarifa ulizonazo kwa makini, usiamini maneno ya watu, nenda mbali zaidi kujiridhisha na kile unachoambiwa au unachoona.
Pili; muda ni silaha yako muhimu. Muda ni tiba ya kila kitu, hakuna kinachoweza kushinda muda. Siku zote kama siyo jambo la kufa na kupona, basi jipe muda. Kwa mambo mengine, jipe muda kabla hujafikia uamuzi kamili.
Tatu; epuka kuendeshwa na hisia. Maamuzi mengi tunayofanya kwenye maisha yetu, yanaendeshwa na hisia. Na hisia kuu zipo mbili, furaha na hasira. Usifanye maamuzi ukiwa na furaha sana au ukiwa na hasira sana, lazima tu utakosea.
Kwa sababu mara zote hisia zinazuia uwezo wetu wa kufikiri kwa kina. Hivyo unapokuwa kwenye hali ya furaha, au hali ya hasira, jizuie kabisa kufanya maamuzi yoyote, utakuja kuyajutia.
Nne; tumia kauli ya Richard Branson. Ni mjasiriamali bilionea wa nchini Uingereza, ana makampuni zaidi ya 400. Kuna kauli yake moja ambayo huwa inasema fursa za kibiashara ni sawa na mabasi ya abiria, mara zote kuna basi jingine linakuja . Kama ambavyo unajua, daladala moja ikipita, basi ipo nyingine inakuja.
Hii ni muhimu kuitumia kuepuka kukurupuka na kuvamia fursa kwa sababu tu watu wanakuambia inapita au hautaiona tena .
Usisumbuke kuingia kwenye fursa ambayo huijui vizuri, fursa zipo nyingi mno.
Hatua ya kuchukua; tunapaswa kufanyia kazi haya Ili kujijengea nidhamu ya kuwa na subira ya kufanya maamuzi makubwa kwenye maisha yetu. Tuepuke kukurupuka kwenye jambo lolote lile na pia tujifunze kwenye kila chochote tunachofanya.
Kila la kheri.
Wako Maureen Kemei,
Rafiki wako.