Rafiki yangu mpendwa watu huwa wanasema ubinadamu ni kazi, lakini siyo kazi ngumu kama ukiishi kwa falsafa sahihi.
Robin Sharma anatushirikisha falsafa sahihi ya kuishi kwenye kitabu cha the daily manifesto ambayo huturudisha kwenye ubinadamu.
Falsafa hiyo ni kuzingatia yafuatayo;
Yaendee maisha kwa moyo uliojaa ushujaa na macho yanayoangalia nguvu kubwa iliyo ndani yako.
Tambua kuna wakati mambo yatakuwa magumu na mabaya, lakini mwisho wa siku maisha ni mazuri.
Kuna watu watakuchukia na kutamani uanguke, wasamehe na watakie mema. Usiruhusu chuki au hasira kuwa ndani yako.
Fanya kazi yako kwa bidii, juhudi na kutoa thamani kubwa zaidi kwa wale wanaopokea kile unachofanya. Heshimu upekee wako na uonyeshe kupitia kazi unayofanya badala ya kwenda na mazoea.
Yafanye maisha kuwa rahisi kwa kuhangaika na vitu vichache vyenye maana na tija kwako. Usihangaike na mengi yanayofanya maisha kuwa magumu.
Toa zaidi ya unavyopokea, kuwa na msaada na huduma kwa wengine na mchukulie kila unayekutana naye kwa heshima.
Furahia kukutana na watu wenye hekima, kusoma vitabu vinavyokuhamasisha na kuwa na mahusiano mazuri na wewe mwenyewe.
Kundi linapokulazimisha uwe kama wao, kataa na baki kuwa wewe halisi, kuwa mkweli kwako.
Kuwa jasiri, ukijua waoga huwa hawawi na maisha bora kwao. Kuhairisha maisha yako ni kukaribisha majuto.
Kumbuka wakati ambapo hofu inakuwa kubwa ndiyo wakati unaukaribia ushindi mkubwa. Na hofu hugeuka kuwa imani pale unapoikabili.
Furahia matunda ya kazi yako, ishi kwa upendo na jali wengine. Fanya haya yote kuungana na ukuu ulio ndani yako na kuwa shujaa wa kweli ambaye ndiyo asili yako.
Hatua ya kuchukua; rafiki yangu tunapaswa kufanyia kazi falsafa hayo na bila shaka tutaishi maisha yenye furaha.
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.