Rafiki yangu mpendwa tunaishi kwenye kipindi ambacho mambo hasi yanapewa nguvu kubwa na ni rahisi sana kukata tamaa. Lakini pia njia za mkato ambazo siyo sahihi zimekuwa nyingi na kuwapoteza wengi. Tunapaswa kuwa na njia ya kujilinda ili kutokukata tamaa na kufanya yaliyo sahihi.
Ili kutokukata tamaa, tunapaswa kujaza akili zetu fikra sahihi za ndoto kubwa ambazo tunazo na kufanya hizo zitutawale muda wote. Kwani akili zetu ni ni kama kisima, kikiwa kitupu, kitajaa uchafu. Kama hakuna fikra sahihi zinazojaa akili yako, fikra za hovyo zitapata nafasi na kukukatisha tamaa.
Kuepuka kufanya yasiyo sahihi jiwekee sheria ya mara zote kufanya kilicho sahihi na siyo kilicho rahisi. Kwa kila unachofanya mbele yako kutakuwa na njia mbili, iliyo sahihi na iliyo rahisi. Na karibu mara zote, kilicho rahisi kufanya huwa siyo sahihi. Hivyo fanya maamuzi yako kwa kuangalia usahihi na siyo kuangalia urahisi.
Siri ya kwanza ya kujenga mtazamo wa uwezekano ni kuwa na kadi ndogo ambayo umeandika kauli au nukuu chanya na inayokupa msukumo mkubwa. Kwenye siku yako, kadiri unavyopata muda soma kadi hiyo na utendelea kubaki chanya na kuwa na msukumo mkubwa.
Mbili pata muda wa kuwa peke yako kuwa na utulivu. Kelele na usumbufu unaotuzunguka kila mahali na kila wakati imekuwa chanzo cha wengi kuvurugwa. Ili kuondokana na hilo, tenga muda utakaokuwa peke yako na kwenye utulivu mkubwa.
Tumia muda huo kufanya tahajudi na kutafakari mambo mbalimbali kwenye maisha yao. Huu ni wakati wa kuwa na wewe mwenyewe, ambao ni muhimu kwa mafanikio yako.
Tatu ni shukuru kwa mnyororo mzima wa thamani. Haijalishi unapitia nini, kuna mambo mengi mazuri yanayoendelea kwenye maisha yako. Shukuru kwa mambo hayo na hilo litakufanya uwe kwenye mtazamo mzuri.
Na usiishie tu kushukuru kile kilicho mbele yako, bali shukuru mnyororo mzima wa thamani. Mfano kama umesafiri salama, shukuru dereve wa gari, waliojenga barabara na wengine wanaohusika kuhakikisha safari inakuwa salama. Kadhalika unaponunua kitu, shukuru mnyororo mzima wa thamani unaowezesha wewe kupata kitu hicho.
Nne ona suluhisho kwenye kila tatizo. Hakuna tatizo ambalo halina suluhisho ndani yake. Hivyo wewe usiwe mtu wa kuangalia tu tatizo, bali angalia ni suluhisho lipi lililo ndani ya tatizo hilo. Kwa kutafuta suluhisho utaliona na kuweza kutatua matatizo mbalimbali yanayokukabili.
Chukua hatua, rafiki yangu usikubali chochote kile kikukatishe tamaa, kuwa na mtazamo wa uwezekano mara zote na utaweza kufanya makubwa.
Mwandishi wako,
Maureen Kemei .
kemeimaureen7@gmail.com