Rafiki yangu mpendwa, bila shaka umekuwa ukisikia kufikiri chanya kunahubiriwa sana kwenye kutengeneza mtazamo sahihi wa mafanikio. Ni kweli kufikiri chanya kuna manufaa kuliko kufikiri hasi, lakini pia pasipokuwa na mpango sahihi, kufikiri chanya kunaweza kuwa tatizo kubwa.
Watu wengi wamekuwa wakitumia kufikiri chanya kama njia ya kukwepa na kujaribu kuzika hisia zao. Pale wanapokutana na tatizo au changamoto na kuibua hisia ndani yao, wanakimbilia kufikiri chanya ili kuondoa hisia hizo.
Kinachotokea ni hisia haziondoki, badala yake zinadidimizwa. Hilo linamtaka mtu atumie nguvu zake nyingi kuendelea kudidimiza hisia hizo ili zisipate nafasi ya kuibuka na kumsumbua.
Sina uhakika kama itakufaa, lakini hivi ndivyo wengi wamekuwa wakitengeneza matatizo ya kisaikolojia kwa baadaye. Unachopaswa kufanya ni kutokutumia hisia zozote unazokuwa nazo.
Badala yake jipe muda wa kukaa na hisia zako, kuzielewa na kuzitatua. Fungua moyo wako na zielewe hisia mbalimbali unazopitia, Ili uweze kuzitatua na kuwa huru nazo. Baada ya kufanya hivyo, hapo sasa unaweza kufikiri chanya utakavyo na hilo litakusaidia.
Tambua hapa haimaanishi utawaliwe na hisia zako na zikusukume kufanya mambo fulani fulani. Bali inamaanisha kuzipa nafasi, kuzielewa na kutatua kile kinacholeta hisia hizo.
Kumbuka hisia zetu zina nguvu kubwa, ukijaribu kuzididimiza, zinazidi kupata nguvu na siku moja zitalipuka na kuleta madhara makubwa.
Hatua ya kuchukua, rafiki yangu tunapaswa kuzikabili hisia pindi zinapokujia, tatua kile kinachozileta na utakuwa huru kiakili na kihisia kitu kitakachokuwezesha kufanya makubwa.
Mwandishi wako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.