Mambo 6 Ya Kujifunza Kutoka Kwa Leonardo Da Vinci.

Rafiki yangu mpendwa Robina anatushirikisha aliyojifunza baada ya kutembelea jumba la makumbusho ya kazi za Leonardo da Vinci ambaye anachukuliwa kuwa mtu mbunifu zaidi kuwahi kuishi hapa duniani.

Wengi waliamini uwezo wake haukuwa wa kibinadamu, bali kulikuwa na uungu ndani yake. Kwani katika kipindi chake alifanya makubwa kwenye sekta mbalimbali kama usanifu, uinjinia, sayansi ya anga na muundo wa viumbe hai.

Robin anatushirikisha tabia sita za Leonardo alizojifunza kutoka kwenye vitabu vyake na ambazo zilimwezesha kuwa mbunifu wa kipekee.

Tabia ya kwanza ni kuandika. Leonardo alikuwa na tabia ya kuandika kila alichofikiria na alichopanga kufanya. Kuandika kulimwezesha kupangilia mawazo yake vizuri na hivyo kuweza kufanya makubwa.

Tabia ya pili ni kutumia udadisi uliokuwa ndani yake. Wote tulipokuwa watoto tulikuwa wadadisi, lakini baada ya kukua tukaacha udadisi huo. Leonardo hakuwahi kuacha udadisi wake, aliendeleza kila alichofanya akiwa na udadisi kama wa mtoto mdogo. Hivyo alikuwa tayari kuuliza maswali na kutafuta majibu, badala ya kujiambia tayari najua.

Tabia ya tatu ni kuwa na subira. Leonardo hakuwa anaharakisha kufanya kazi zake, alijipa muda wa kutosha katika kufanya kazi zake na hilo lilimwezesha kuzalisha matokeo makubwa.

Wakati anachora moja ya picha zake maarufu sana ya chakula cha mwisho cha Yesu, alikuwa anaweza kuangalia picha kwa siku nzima bila kufanya chochote, kisha akafanya marekebisho machache na kuondoka. Lilimchukua muda mrefu kukamilisha picha hiyo, lakini ni picha maarufu kuliko zote duniani.

Tabia ya tano alitenga muda wa kupumzika. Leonardo hakuweka muda wake wote kwenye kazi, badala yake alijipa muda wa kupumzika na kutembea maeneo mbalimbali. Hilo liliipa akili yake mapumziko ambayo yalichochea zaidi ubunifu. Na pia katika matembezi yake, ndipo alipata mawazo mapya ya kufanyia kazi.

Ubunifu unahitaji mtu ayaishi maisha kwa ukamilifu wake na siyo kufanya kazi muda wote na kuichosha akili mpaka inashindwa kuja na ubunifu mzuri.

Tabia ya sita ni kupenda uzuri wa asili. Leonardo alitumia muda wake mwingi kutembea kwenye asili, sehemu ambayo alipata mawazo mazuri na ya kibunifu. Kwa kuona uzuri wa asili na utulivu mkubwa wanaokuwa nao, mawazo ya kibunifu yanakuja kwao kwa urahisi.

Chukua hatua, hata wewe rafiki yangu unaweza kujijengea ubunifu kama Leonardo, unachohitaji ni kujijengea tabia hizo sita.

Mwandishi wako,

Maureen Kemei.

kemeimaureen7@gmail.com.

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *