
Rafiki yangu mpendwa watu wengi wamekuwa wakifanya mambo kwa ajili ya kujijengea sifa baada ya kuondoka hapa duniani.
Wanafanya kwa lengo la kuendelea kukumbukwa vizazi kwa vizazi kwa majina yao kuandikwa maeneo muhimu au kuchengewa masanamu.
Lakini kama ilivyo kwenye mambo mengine ya maisha, unapolazimisha kitu, huwa hakitokei.
Unapofanya mambo ili ukumbukwe, hakuna anayekukumbuka, kwa sababu unakuwa siyo halisi.
Achana na msukumo wa kufanya kitu ili kukumbukwa au kuacha alama. Badala yake chagua kuishi maisha halisi kwako, simamia kile kweli unachoamini na utakuwa na maisha bora huku pia ukiwa na nafasi kubwa ya kuendelea kukumbukwa.
Watu hawatakukumbuka kwa sababu unataka wakukumbuke, bali watakukumbuka kwa aina ya maisha unayoishi. Hivyo wajibu wako mkubwa ni kuyaishi maisha yako kwa uhalisia na ukamilifu.
Furahia pale mambo yanapokwenda vizuri na kuwa na shukran yanapokwenda vibaya.
Waelewe wale wanaokuzunguka na wasamehe wale wanaokuumiza. Ichukulie kazi au biashara yako kwa heshima kubwa na toa thamani kubwa kwa wengine.
Chagua kuwa wewe na kusimamia kile kilicho sahihi hata kama wengine wote wanapingana na wewe.
Kuwa mnyenyekevu kadiri unavyofanikiwa na endelea kuifanya dunia kuwa bora zaidi.
Jifunze kutokuweka uzito kwenye mambo madogo madogo na jua mengi unayohofia hata haitatokea.
Chukua hatua; rafiki chagua kuyaishi maisha yako halisi wakati huu ukiwa hai na usijisumbue na nini kitatokea baada ya kuwa umekufa.
Utakuwa chakula cha mchwa na mbolea ya ardhi. Namna ulivyoishi maisha yako ndiyo itaacha alama hapa duniani.
Rafiki yako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com