Rafiki yangu mpendwa ili uweze kufanya makubwa, lazima kwanxa utoke kwenye hali ya uathirika kwenda kwenye hali ya ushujaa.
Hili ni zoezi ambalo linapaswa kuanzia ndani yako, zoezi ambalo siyo rahisi, lakini ukilifanya utapiga hatua kubwa.
Hatua ya kwanza; Ondoka kwenye mtazamo wa haiwezekani kwenda kwenye mtazamo wa inawezekana. Waathirika huwa wanaona mambo hayawezekani wanaona kikwazo kwenye kila jambo na hilo kiwazuia kuchukua hatua na kufanya makubwa.
Mashujaa Wana mtazamo wa tofauti, wanaona mambo yote yanawezekana na hakuna kinachowazuia kupata wanachotaka. Hilo huwasukuma kuchukua hatua na kufanya makubwa.
Hatua ya pili; Acha kutoa sababu na anza kutoa matokeo. Unaweza kutoa sababu au kutoa matokeo, huwezi kutoa vyote kwa pamoja. Waathirika hutoa sababu kwa kila jambo kuonesha kwamba haiwezekani.
Mashujaa huwa wanatoa matokeo, hawahangaiki kutafuta sababu na visingizio, bali wanazalisha matokeo. Kwa njia hiyo wanafanya makubwa bila kujali wanapitia nini.
Hatua ya tatu; Acha kuishi jana, tengeneza kesho bora. Waathirika huishi kwenye wakati uliopita na kutumia yale yaliyotokea uko nyuma kama sababu ya wao kuwa pale walipo sasa.
Mashujaa wanapambana kujenga kesho iliyo bora wakitumia waliyopitia uko nyuma kama somo na msukumo wa kufanya makubwa zaidi.
Hatua ya nne; Acha kuwa bize, zalisha matokeo. Waathirika wanapenda kuwa bize, kwa sababu wanaona hilo ni sifa. Siku yao nzima imejaa mambo ya kufanya, lakini mengi katika hayo siyo muhimu.
Hawana vipaumbele vyovyote hivyo, lakini wanaimaliza siku wakiwa wamechoka, lakini hakuna matokeo makubwa wanayozalisha.
Mashujaa wanajua kinachohitajika ni kuzuia matokeo muhimu , hivyo hupangilia muda na kuweka vizuri vipaumbele vyao. Hilo huwawezesha kufanya vizuri machache yaliyo muhimu na yenye tija, kitu kinachowapa matokeo makubwa.
Hatua ya Tano; Acha kuwa mchukuaji na anza kuwa mtoaji. Waathirika huwa na mtazamo wa uhaba . Wanaona rasilimali muhimu ni chache na zipo kwa uhapa, hivyo hukazana kupata zaidi ya wengine. Mtazamo huo hugeuka kuwa kikwazo kwao wasipate mafanikio makubwa.
Mashujaa wana mtazamo wa utele, wanajua rasilimali muhimu zipo kwa uwingi kiasi cha kila mtu kuweza kupata kadiri anavyopata.
Na wanajua ili wapate wanachotaka, wanapaswa kuwapa kwanza wengine kile wanachotaka. Na kadiri wanavyotoa, ndivyo wanavyopata zaidi na zaidi.
Chukua hatua, rafiki kazi kwetu kuweka kwenye matendo haya ambayo tunajifunza siku ya leo, ili tutoke kwenye mtazamo wa uathirika kwenda kwenye mtazamo wa hero.
Rafikk yako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com