Jinsi ya kubali yaliyo nje ya uwezo wetu.

Rafiki yangu mpendwa kwenye falsafa ya ustoa, kuna dhana moja ambayo inaitwa amori fati ikiwa na maana kwamba, ipende hatima yako yaani love your fate.

Maana ya kubwa ya dhana hii kwenye falsafa ya ustoa ni kwamba wastoa waliamini tunapaswa kupokea kila kitu kinachotokea kama vile tulitaka kitokee.

Hii ina maana kwamba, chochote kile kinachotokea, kwanza unakipokea na kukikubali kisha unachukua hatua kuhakikisha kinakuwa na manufaa kwako.

Kukataa kukubali na kupokea yale yaliyo nje ya uwezo wako ni kukubali kuumizwa zaidi na pia ni kuchagua kuwa kiranja wa dunia. Kuwa kiranja wa dunia ni kazi kubwa na ipo nje ya uwezo wa binadamu kabisa.

Kwa kukubali yale yaliyo nje ya uwezo wako unajipa nafasi ya kuweza kuyavuka yasiwe kikwazo kwa mafanikio yako.

Sina uhakika kama itakufaa, lakini kwenye falsafa ya ustoa kuna upacha wa kila kitu, kama kuna mazuri basi unapaswa kujua kuwa kuna mabaya pia. Pale leo unapopitia na kufurahia mazuri jua kuwa kuna siku utakuja kupitia mabaya pia.

Kupenda hatima yako ni kukabiliana na yote ambayo asili imeamua juu yako na wala siyo kulalamika.

Kwenye maisha maumivu huwa hayakosekani, kuna mambo mengi huwa yanakwenda kinyume na matarajio yetu.

Lakini mateso ni kitu ambacho mtu unajichagulia mwenyewe. Unachagua mateso pale unapojaribu kukataa kile kinacholeta maumivu (yaani kujaribu kuwa kiranja wa dunia).

Ukikubali kile kinacholeta maumivu unaacha kuteseka na kuona hatua zipi sahihi za kuchukua. Kwa kila unalokutana nalo kwenye maisha yako linaweza kuwa ndani ya uwezo wako kudhibiti au nje ya uwezo wako.

Kuchukua hatua; rafiki yangu kwa yaliyo ndani ya uwezo wako chukua hatua sahihi katika kukabiliana nayo. Na usikubali kilicho nje ya uwezo wako kuwa kikwazo kwako, kikubali kisha kivuke Ili uweze kufanikiwa.

Kitu kimoja zaidi ni kwamba kamwe usikubali kuwa kiranja wa dunia, kwani huko ni kukubali kujiumiza kwa kutaka kufanya yaliyo nje ya uwezo wako.

Rafiki yako,

Maureen Kemei.

kemeimaureen7@gmail.com.

uamshobianfsi.com.

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *