Tambua kwamba huwezi kupata muda, bali unapaswa kutenga muda. Kama kitu ni muhimu, unatenga muda wa kukifanya . Hapa unahitaji kuweka vipaumbele vyako sawa.
Tambua ukweli huu kwamba hulazimiki kufanya chochote kile. Kila unachofanya na muda wako, umechagua mwenyewe. Hakuna aliyekushikilia bastola na kukuambia usipofanya hivi nakuua. Umechagua mwenyewe hivyo mamlaka ni yako, unaweza kuchagua kwa namna nyingine kama ulivyochagua sasa haikuridhishi.
Pima matumizi yako ya muda kwa sasa. Chukua siku saba na orodhesha yote unayofanya kwenye muda wako. Zoezi hilo litakuonyesha wapi muda wako unapotelea zaidi na hivyo kuweza kuuokoa.
Lenga kupata masaa mawili huru kila siku. Baada ya kuorodhesha yote unayofanya kwenye siku yako, angalia ni yapi ambayo hayana tija na yafute. Lengo ni uweze kupata angalau masaa mawili kila siku, ambayo unaweza kuyatumia kwa yale muhimu unayochagua.
Kwa nini masaa mawili? Moja kwa kuwa itakusukuma kuondoa ukomo ulionao. Na mbili kwa sababu ukiyawekeza vizuri masaa hayo mawili kila siku, utaweza kufanya makubwa.
Tambua kila ndiyo ni hapana . Unaposema ndiyo kwenye jambo moja, maana yake unasema hapana kwenye jambo jingine . Kwa kuwa na masaa 24 tu kwa siku, lazima uchague kwa umakini mambo gani yakusema ndiyo na yapi yakusema hapana.
Ondoka kwenye mazoea. Kinachofanya ukose muda ni mazoea ambayo tayari umeshajijengea .Kuna aina ya maisha umeshayajenga kwako ambapo kuna vitu unafanya kama sehemu ya maisha yako.Ni wakati wa kuyamulika maisha yako na kuvunja kila mazoea yanayokupozea muda. Hili halitakuwa rahisi maana litaathiri wengine, lakini lazima ulisimamie.
Kupata muda zaidi, fanya haya; acha kuangalia tv, kusoma magazeti, na kuzurura kwenye mitandao ya kijamii.
Tenga muda wa kujibu simu, jumbe na barua pepe, usiruhusu hivyo kuwa usumbufu kwako muda wote.
Andaa na kula vyakula bora kwa afya yako. Hilo litapunguza muda na uchovu.
Jilazimishe kupata muda. Kama bado unaona huwezi kupata muda, jua ni ukomo tu unakuambia hivyo na siyo ukweli.
Pata picha umeumwa sana, ukaanguka na kupoteza fahamu, ukapelekwa hospitali na kulazwa kwa wiki nzima.
Baada ya vipimo mbalimbali, daktari anakuambia una ugonjwa ambao tiba yake pekee ni kila siku utenge masaa mawili ya kukaa kwa utulivu bila ya kufanya chochote.
Na kama siku itapita hujatenga masaa hayo mawili, utaumwa na kuzimia tena na ukizimia mara ya pili uwezekano wa kufa ni mkubwa.
Sasa niambie, hutayapata masaa mawili kwa siku? Jibu liko wazi, utayapata tu. Hivyo muda upo, ni wewe kujisukuma uweze kuutenga na kuutumia vizuri.
Rafiki yako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.