Rafiki yangu mpendwa hofu ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Kila mtu huwa anakutana na hofu, hasa pale unapofanya kitu kipya ambacho hujazoea kufanya.
Kila mtu huwa anahofia, kila anayefanya kitu kwa mara ya kwanza anakuwa na hofu kubwa. Hata wale wanaoonekana ni majasiri, ndani yao huwa wanakuwa na hofu kubwa.
Lakini huwa wanaweza kuzishinda hofu hizo. Mabadiliko makubwa ya kimtazamo unayopaswa kuyafanya ili uishinde hofu ni kujua kwamba hofu siyo adui.
Hofu siyo kitu ambacho kinalenga kukuangusha na kukushinda. Hofu ni tahadhari ambayo akili yako inakupa, kwa lengo zuri tu la kuhakikisha unakuwa hai na salama.
Sina uhakika kama itakufaa, lakini hofu ndiyo imekiwezesha kizazi chetu binadamu kuendelea kuwa hai mpaka leo. Ni kwa sababu hofu inaleta tahadhari na mtu anapochukua tahadhari hiyo anakuwa salama.
Hivyo tunapaswa kuchukulia hofu siyo kama kikwazo cha kutufanya tusimame, bali kama tahadhari ya kwenda kwa umakini.
Habari njema ni kuwa huhitaji kuvunja kabisa hofu ndiyo uweze kufanya makubwa. Unachopaswa kufanya ni kujisikiliza, kuielewa na kuchukua hatua huku ukiwa na tahadhari.
Hofu huwa inaonekana ina nguvu kwa sababu inagusa zaidi hisia zetu. Na pale kitu kinapogusa hisia, huwa tunakipa uzito zaidi.
Kwa kuweza kuisikiliza na kuielewa hofu, utaweza kuchukua hatua sahihi na kufanya makubwa. Chukua mfano unataka kuanzisha biashara, lakini unahofia itashindwa . Hiyo haimaanishi kwamba ni uhakika biashara hiyo itashindwa, bali ni tahadhari kwamba upo uwezekano mkubwa wa biashara kushindwa.
Hivyo unapaswa kuendesha biashara yako kwa umakini mkubwa ili kuepuka hatari za kushindwa.
Kuchukua hatua ndiyo njia pekee ya kuishinda hofu yoyote unayokuwa nayo. Njia pekee ya kuivuka hofu ni kuchukua hatua kufanya kile unachohofia kufanya.
Baada ya kuisikiliza na kuielewa hofu, unapaswa, kuchukua hatua. Usiendelee tu kuitafakari, badala yake chukua tahadhari ambazo hofu inakupa na kisha chukua hatua.
Unapochukua hatua na kupata matokeo mazuri, unazidi kujiamini na kupata hamasa ya kuchukua hatua zaidi.
Hata pale hofu inapokuwa kali na ukashawishika uache kufanya, usisikilize hofu, badala yake chukua hatua. Hata kama itakuwa hatua ndogo kiasi gani, una nguvu ya kuivuka hofu yoyote unayokuwa nayo.
Kama unataka kumuuliza mtu kitu na unahofia, jua ni tahadhari gani hofu inakupa kisha muulize mtu huyo kile unachotaka kumuuliza.
Utashangaa jinsi hilo linavyokuwa rahisi kwako na mtu huyo anakujibu vizuri kuliko hata ulivyotegemea.
Na hata kama hatakujibu vizuri, bado hakuna hatari kubwa au chochote ulichopoteza kwa kuuliza.
Hofu pia ni nzuri pale inapokuzuia usifanye mambo yenye madhara kwako. Kama unahofia madeni, unakuwa na nidhamu nzuri ya fedha.
Kama unahofia magonjwa sugu unalinda afya yako. Kwa kuitazama vizuri, hofu ni rafiki yako mkubwa, anayekujali na kutaka kuona upo salama.
Chukua Hatua; rafiki yangu tunapaswa tuielewe hofu na kuchukua hatua sahihi. Kamwe tusikubali hofu ituzuie kwenye kuchukua hatua.
Mwandishi wako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.