Gereza Ambalo Mtu Unatembea Nalo.

Mabadiliko makubwa ya teknolojia yaliyotokea miaka zaidi ya kumi iliyopita ni ujio wa simu janja smartphones, kifaa chenye uwezo mkubwa kama kompyuta na mtu unatembea nacho kila mahali.

Kifaa hicho ni gereza mbalo mtu unatembea nalo kwa sababu kumekuwa kinatumika kukubadilisha tabia ili uendane na matakwa ya watu wachache wanaotaka kujinufaisha na kufaidika kupitia wewe.

Kifaa hicho kinakuletea mapendekezo madogo madogo ambayo yanabadili kabisa maisha yako huku wewe ukiwa hujui kinachofanyika.

Mwandishi wa kitabu cha ten arguments for deleting your social media accounts right now, anasema kifaa hiki kimetugeuza watu kuwa kama wanyama wanaofanyiwa majaribio kwenye maabara.

Mitandao ya kijamii ina mfumo wa kukusanya taarifa Algorithms ambayo inakusanya taarifa nyingi za kila aina ambacho kila mtu anafanya akiwa kwenye mitandao hiyo.

Umewahi kuangalia video moja mtandaoni kisha ukaletewa video nyingine nyingi zinazofanana na hiyo? Hapo jua mfumo huo unafanya kazi.

Algorithms ni mfumo mkubwa unofanya kazi kila wakati na kukusanya taarifa zako zote za matumizi ya mitandao hiyo. Ukifungua kiungo cha aina fulani, mfumo unachukua taarifa, kama unaendelea kuangalia picha au video za aina fulani taarifa zako zinachukuliwa.

Mfumo hiyo ina uwezo mpaka wa kujua ni wakati gani una furaha, wakati gani una huzuni na taarifa nyingine nyingi.

Sasa pata picha mfumo huo inakusanya taarifa za mabilioni ya watumiaji ya mitandao hiyo, kisha kuzichakata kulingana na umri wa mtu, jinsia, alipo na taarifa zake nyingine nyeti anazokuwa ameweka kwenye mitandao hiyo.

Kuwa na taarifa nyingi za mtu kunaipa mifumo hiyo nguvu ya kukushawishi bila ya wewe kujua. Kwa sababu inakuwa inakujua kuliko unavyojijua wewe mwenyewe.

Lakini kumbuka mfumo huo haujaja kwako kukulazimisha uupe taarifa, ni wewe mwenyewe unaupa taarifa kwa kila unachofanya kwenye mitandao hiyo.

Na ukishaupa mfumo taarifa za kutosha, unakuwa umeupa nguvu ya kukushawishi, unajikuta unafanya vitu ukifikiri umeamua mwenyewe, kumbe umeshawishiwa.

Mfano, mfumo umejifunza kuwa ukiwa na huzuni unaangalia video za aina fulani, hivyo ukianza kuangalia video hizo, mfumo unakuletea tangazo ambalo litakushawishi zaidi kwa kuwa huzuni. Utajikuta unafanya maamuzi bila ya utashi wako.

Hii ni hatari kubwa ambayo wengi hawaijui, lakini mambo mengi ambayo watu wanafanya wameshawishiwa na mitandao wa kijamii bila wao kujua. Ndiyo maana mwandishi anasisitiza sana, njia pekee ya kuepuka hili ni kuacha kabisa kutumia mitandao hiyo.

Maana hata ukisema unatumia kwa kujidhibiti, bado mfumo unakusanya taarifa zako nyingi kila unapotumia na kuzitumia kukushawishi ufanye maamuzi yenye manufaa kwa wengine na siyo kwako.

Mitandao ya kijamii huwa inakusanya taarifa za watumiaji wake na kisha kuziuza kwa wale wanaotaka kutangaza biashara zao kupitia mitandao hiyo.

Matangazo yanakuwa na ushawishi mkubwa kwa sababu yanakuwa yanamlenga moja kwa moja mtu ambaye yuko kwenye hali ya kushawishika haraka, mtu ambaye utashi wake haupo huru tena.

Unapotumia mitandao hii, huna tofauti na panya anayefanyiwa majaribio kwenye maabara. Wewe unafanyiwa majaribio ya kiutashi, kwa kufuatiliwa kwa muda mrefu, tabia zako kujulikana na kisha kuletewa matangazo yanayokuwa na ushawishi mkubwa kwako, bila ya kujua kama ni matangazo.

Asante,

Rafiki wako,

Maureen Kemei .

kemeimaureen7@gmail.com

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *