Uraibu Unavyozalisha Tabia Mbaya.

Rafiki yangu mpendwa uraibu wa aina yoyote ile, huwa unabadili tabia ya mtu kabisa. Mtu akishakuwa na uraibu hawezi tena kufikiria, anakuwa kama msukule.

Yuko tayari kufanya chochote bila kujali madhara yake, hili tu kukamilisha hitaji la uraibu wake.

Mfano mzuri ni wateja wa madawa ya kulevya wanapotaka kupata madawa, wapo tayari kufanya chochote ili kukamilisha hilo.

Hivyo pia ndivyo mitandao ya kijamii inavyobadili watu, inawafanya wawe na uraibu wa mtandao hiyo kisha kuwasukuma kupata kile wanachotaka bila kujalia madhara yake.

Kuna baadhi ya tabia ambazo zimekuwa zinaoneshwa na waraibu wa mitandao ya kijamii ambazo zina madhara kwao na kwa wengine, lakini hawajali. Tabia hizo ndizo zinainufaisha zaidi mitandao hiyo.

Baadhi ya tabia hizo ni:

  1. Ubinafsi wa mtu kujiangalia mwenyewe bila kujalia wengine.
  2. Hofu na wasiwasi uliopitiliza kwa kitu kisichoonekana na wengine.
  3. Kiburi na dharau kwa wengine. Watu wakishakuwa na uraibu wa mitandao wa kijamii na kuwa na wafuasi wengi hupata kiburi na kujiona wako juu kuliko wengine.
  4. Kuamini vitu visivyosahihi au uhalisia. Imani za nadharia za uongo conspiracy theories zimekuwa zinasambazwa kwa kazi kupitia mitandao ya kijamii.
  5. Kwa kuwa mtu anateseka na uraibu wake, anahakikisha anawatesa wengine pia. Watu wamekuwa wanatumia mitandao ya kijamii kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wengine hasa wanapokuwa wanajua udhaifu wao.

Mwandishi wa kitabu cha ten arguments for deleting your social media accounts right now, anatupa mfano wa aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump ambaye alikuwa anatumia sana mtandao wa Twitter, ambapo kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda ndivyo alivyokuwa ana uraibu na mtandao huo na kuwa na tabia za hovyo.

Hiyo ilipelekea Twitter na mitandao ya kijamii kumfungia kabisa, lakini ni baada ya mitandao hiyo kuwa imenufaika na uwepo wake vya kutosha na kuona hawezi kuwa na manufaa kwao tena baada ya kushindwa kwenye uchaguzi.

Kwa kuangalia sakata la Trump na mitandao ya kijamii, tangia uwepo wake mpaka kufungiwa kwake, ni sababu tosha kwa nini kila mwenye akili timamu anapaswa kuachana kabisa na mitandao hiyo.

Rafiki yako,

Maureen Kemei.

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *