Rafiki yangu mpendwa watu wengi husema kitu kikubwa ambacho kila mtu anahofia ni kifo, hilo siyo kweli. Kitu kikubwa ambacho kila mtu anahofia ni kuishi maisha yake kwa uhalisi wake.
Watu wengi hawana uthubutu wa kuchagua kuyaishi maisha yao kwa namna wanavyochagua wao, hivyo wanalazimika kujificha kwenye utumwa wa jamii.
Tumefundishwa kuyaishi maisha yetu ili kuwaridhisha wengine, wakubaliane na sisi na kutuona ni watu wazuri, hata kama inabidi tuigize maisha ili kukamilisha hilo. Tumezoea kuishi kama wengine wanavyotaka tuishi ili wakubaliane na sisi.
Kuchagua kuwa wewe na kuyaishi maisha yako kwa namna unavyochagua mwenyewe ni kitu ambacho watu wanakihofia zaidi kuliko hata kifo. Wengi wapo tayari wafe kuliko kuchagua kuyaishi maisha yao.
Maisha ambayo wengi wanaishi siyo maisha halisi kwao, bali ni maisha ambayo wengine wanawategemea wawe hivyo. Dini ambazo wengi wanazo, kazi wanazofanya na maisha wanayoishi, siyo kwa sababu wamechagua wenyewe, bali kwa sababu ndivyo jamii inawategemea wawe. Kwa njia hiyo wengi wanaishi maisha yasiyo yao, maisha ya utumwa.
Kwa kuwa maisha ambayo watu wanaishi siyo yao, wanaacha kujiheshimu na kujiamini . Wanajiona ni watu ambao hawajakamilika na hivyo kuzidi kutafuta njia za kuwafurahisha wengine, hapo wanazidi kuwa watumwa zaidi kwenye jamii.
Watu wamekuwa wanajidharau wao wenyewe ili kuwafurahisha wengine.. Wamekuwa wanajiumiza miili yao ili tu kuwafurahisha na kukubalika na wengine. Angalia vijana wanaoingia kwenye ulevi na madawa ya kulevya, siyo kwa sababu vina manufaa kwao, ila kwa sababu wanataka wakubaliane na wengine.
Hata watu wazima kuna mambo wanafanya ambayo hayana manufaa kwao na tena yanawaumiza, lakini wanataka wakubalike na wengine.
Watu wanajiumiza na kutokujikubali kwa sababu hawana uthubutu wa kuyaishi maisha yao. Wanajiadhibu na kuruhusu wengine wawaadhibu ili tu wakubalike ndani ya jamii. Hili limewafanya wengi kuendelea kubaki kwenye utumwa.
Chukua hatua ; rafiki tunapaswa kuishi maisha halisi, kwa sababu kuishi maisha ya kufurahisha wengine ni kujitesa na kupotezauda wako hapa duniani.
Rafiki Yako,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com