Rafiki yangu mpendwa Punda akiwekewa nyasi upande mmoja na maji upande wa pili, anajikuta njia panda. Anakuwa anataka ale nyasi na pia anywe maji.
Hivyo atabaki hapo akiangalia ni jinsi gani anaweza kupata vyote kwa pamoja.
Kinachotokea ni anajikuta anakufa kwa njaa na kiu wakati amezungukwa na nyasi na maji.
Ambacho punda anashindwa kujua ni kwamba, japo hawezi kufanya vyote kwa pamoja, anaweza kuanza na kimoja kisha kwenda kwenye nyingine.
Kabla hujamshangaa punda kwa kufa na njaa huku akiwa na nyasi, hebu rudi kwako, ni fursa ngapi nzuri zimekuzunguka? Na je, katika fursa hizo ni ngapi unazifanyia kazi?
Watu wengi hasa kwenye zama hizi za mafuriko ya fursa wanajikuta hawafanyi chochote. Wanafursa tano mbele yao na wanataka kuzifanyia kazi zote, kitu ambacho hakiwezekani, hivyo wanaishia kutokufanya chochote.
Suluhisho kwenye hali hiyo ni rahisi ni wewe kuchagua fursa moja na ifanyie kazi mpaka itakapokamilika, kisha nenda kwenye fursa nyingine.
Hata kama una fursa tano mbele yako, ukiipa kila fursa miaka mitano ya kufanyia kazi kwa uhakika, utapiga hatua kubwa kuliko kusubiri mpaka uweze kufanyia kazi zote kwa pamoja.
Chukua hatua, katika fursa zote zinazokuzunguka, chagua moja utakayoifanyia kazi kwa uhakika na kusema hapana kwa nyingine mpaka utakapoikamilisha hiyo. Kisha nenda kwenye fursa nyingine kwa mpango huo huo.
Muda utakwenda iwe utachukua hatua au la. Hivyo badala ya kupoteza muda, chukua hatua.
Rafiki yako,
Maureen Kemei.