Rafiki yangu mpendwa kuna mambo mengi uliyojifunza siku za nyuma ambayo kwa sasa siyo sahihi tena. Muda unakwenda kasi na mambo yanabadilika.
Imani zilizokuwa sahihi huko nyuma sasa siyo sahihi tena. Njia zilizokuwa sahihi na nzuri uko nyuma kwa sasa siyo sahihi tena. Kuendelea kung’ang’ana na mambo ya nyuma, kwa sababu tu yalikuwa na manufaa kwa wakati huo siyo sahihi.
Unapaswa ufike mahali na kubadili yale uliyojifunza. Uondoe yale yaliyopitwa na wakati na ambayo kwa sasa siyo sahihi tena na uweke ambayo yanakwenda na wakati na ni sahihi kwa wakati huu.
Kilichokufikisha hapo ulipo sasa siyo kitakachokufikisha mbele zaidi. Hivyo mara zote kuwa tayari kujifunza vizuri vipya na kuboresha zaidi.
Ili kukamilisha hilo, unapaswa kufuata hatua hizi tatu;
- Kuwa na mashaka na kile unachojua, usijipe uhakika kwenye kitu chochote.
- Acha tabia ya kujiambia tayari unajua kitu, kuwa tayari kujifunza upya, hata kama tayari unajua.
- Kwa kila unachojua tafuta uthibitisho kwamba bado ni sahihi mpaka sasa. Kama siyo sahihi kibadili.
Chukua hatua, kama huendelei kujifunza kila siku, tena kwa makusudi kabisa, hutaweza kukua na badala yake utakuwa unarudi nyuma.
Dunia inakwenda kasi, kuweza kwenda nayo kasi lazima uwe tayari kuacha vile uliyojifunza huko nyuma na kujifunza vipya zaidi.
Rafiki yako,
Maureen Kemei.