Habari
Tunaendelea na uchambuzi wa kitabu cha high performance habits, how Extraordinary people become that way. Kilichoandikwa na kocha Brendon Burchard.
Leo tunaangazia tabia ya pili ya kati ya tabia sita ambazo Brandon anatushirikisha, zitakazotuwezesha kufikia ubobezi na mafanikio kwa ujumla, nenda nami taratibu tupate kuielewa tabia hizi ahsante.
KUTENGENEZA NGUVU.
Mafanikio yako ni matokeo ya nguvu ulizonazo. Huwezi kufanikiwa kama huna nguvu, kwa sababu safari ya mafanikio siyo rahisi kama wengi wanavyofikiri.
Kitu ambacho wengi hawajui ni kwamba nguvu hazitokei tu kwenye maisha, bali zinatengenezwa. Jinsi unavyoendesha maisha yako, kuanzia Kulala kwako ulaji na hata matumizi yako ya muda wa siku yana athari kubwa sana kwenye nguvu zako.
Pia tunapozungumzia nguvu, wengi hufikiria nguvu za mwili pekee, lakini nguvu zinahusisha pia akili na hisia pia. Unaweza kuwa na nguvu nyingi za mwili, lakini akili ikawa haina nguvu na usiweze kuchukua hatua. Au mwili na akili vikawa na nguvu huna hamasa kabisa kwa sababu nguvu za kihisia unakuwa huna.
Ili ufanikiwe sana, unahitaji kuwa na kiwango kikubwa cha nguvu kimwili, kiakili na kiroho (hisia). Na nguvu hizi zinatengenezwa kwa jinsi unavyoendesha maisha yako.
Hatua tatu za kuchukua ili kutengeneza nguvu zaidi kwenye maisha yako.
Moja,achia msongo weka nia.
Msongo wa mawazo ni sumu kubwa Sana kwenye nguvu zako, ni kitu kinachoua kabisa nguvu yoyote uliyonayo ndani yako.
Na msongo wa mawazo umekuwa hautokei tu, bali tumekuwa tunauzalisha kwa jinsi tunavyoendesha maisha yetu. Na tunatengeneza sana msongo pale
Kwenye kufanya kitu kimoja kwenda kufanya kitu kingine.
Ili kuepuka kupoteza nguvu, tunapaswa kuchukua hatua ya kuachia msongo na kuweka nia kila tunapobadili kile tunacho fanya.
Pale unapotoka kufanya kitu kimoja kwenda kufanya kingine, usiingie tu moja kwa moja kwenye kufanya. Badala yake funga macho yako kwa dakika moja au mbili, jiambie maneno, “naachia msongo” kwa kurudia rudia huku ukiuweka mwili wako kwa namna ya kuachia kilichopo.
Unaposikia msongo umetoka kwenye mwili wako, Weka nia ya kile unachokwenda kufanyia kazi. Fikiria ni hisia gani unataka kuwa nazo kwenye kufanya kitu hicho na matokeo unayotegemea kupata.
Kwa kufanya zoezi hili litakalokuchukua dakika 2 mpaka 5 utapata nguvu kubwa ya kuingia kwenye kitu kipya huku ukiachana na msongo wa kile ulichomaliza kufanya.
Mbili, tengeneza furaha.
Furaha ni kitu ambacho tunakitengeneza au kukipoteza sisi wenyewe, siyo kitu ambacho kinatokea au kutafutwa. Kutengeneza furaha yako mwenyewe ni moja ya aina za kutengeneza nguvu zaidi kwenye maisha yako. Kwani unapokuwa na furaha unakuwa na hamasa zaidi ya kuchukua na kupiga hatua.
Unatengeneza furaha kwa kuwa na hisia chanya kwenye maisha yako. Kupenda kile unachokifanya, kuwapenda wengine, kuwa mtu wa Shukrani ni hisia chanya ambazo zinakuletea furaha zaidi.
Pia unatengeneza furaha kwa kutawala akili yako na fikra chanya za yale mazuri unayotaka na kutengeneza taswira ya matokeo unayotaka kupata na kujikumbusha taswira hiyo mara kwa mara.
Tatu,boresha afya yako.
Afya ni eneo muhimu sana la nguvu zako. Bila ya afya imara huwezi kuwa na nguvu. Ili kuboresha afya yako unahitaji kuweka mkazo kwenye maeneo haya matati muhimu.
Eneo la kwanza ni ulaji, kula kwa afya, kula kwa kiasi na kula vyakula ambavyo siyo sumu kwako. Epuka kabisa sugari , ni kitu ambacho kinakuondolea nguvu kwa haraka sana. Kula kiwango kidogo cha wanga, kula mafuta, protini na mboga mboga kwa wingi.
Eneo la pili ni ufanyaji wa mazoezi, kazi za wengi sasa zinahusisha kukaa kwa muda mrefu, kama hufanyi mazoezi, ukaaji wako unapoteza nguvu. Hivyo kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi angalau kwa nusu saa kila siku. Unapofanya mazoezi, mwili unatumia vyakula ilivyohifadhi kuzalisha nguvu zaidi.
Eneo la tatu ni Kulala.
Usingisi ni kiungo muhimu sana cha nguvu zako. Kama hupati usingizi wa kutosha huwezi kuwa na nguvu, kila wakati utajiona umechoka kimwili na kiakili. Tafiti zinaonesha mtu anahitaji masaa 7 mpaka 8 ya kulala ili kuweza kupumzika vizuri. Hivyo Pata usingizi wa kutosha ili kuwa na nguvu.
Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa ushauri nasaha na maisha kwa ujumla. Pia anayejifunza kazi ya uandishi kupitia kwa waandishi wengine.
Maureen Kemei
Email
Kemeimaureen32@gmail.com
Blog kufikirichanya.wordpress.com