Habari
Karibu Mwana mafanikio tumalizie leo tabia ya sita, ambayo tumekuwa tukijifunza mfululizo. Brandon Burchard anatushirikisha tabia hizi, kwenye kitabu chake cha high performance habits (how extraordinary people become that way).
Baada ya kuwakochi watu wenye mafanikio makubwa. Naamini nasi tukichukua hatua hizi kwa kufanya tabia hizo kila siku, kwa kweli safari yetu ya mafanikio itazaa matunda.
Tabia ya sita ;onyesha ujasiri.
Safari ya mafanikio siyo safari rahisi, ina magumu na vikwazo vingi. Kuna kila hatari ya kushindwa kwenye safari hii na hatari hizi zimewazuia wengi Kuendelea na safari hii ya mafanikio.
Njia pekee tunayoweza Kuendelea na safari hii na kufanikiwa ni kwa kuonesha ujasiri. Tunahitaji ujasiri hili tuweze kufanikiwa zaidi.
Na ujasiri haimaanishi kwamba hatuna hofu kabisa, badala yake ni kuwa tayari kuchukua hatua licha ya kuwa na hofu. Wale wanaoonekana jasiri na mashujaa siyo kwamba hawana hofu, wanakuwa nazo, ila hawaruhusu hofu hizo ziwe kikwazo kwao.
Pia ujasiri unaambukizwa, kadiri unavyochukua hatua za kijasiri kwenye eneo moja la maisha yako, ndivyo unavyoweza kutumia kwenye maeneo mengine pia. Hivyo kama huna ujasiri unaweza kuanza na vitu vidogo na kupata ujasiri wa kufanya vikubwa pia.
Ujasiri haupo tu kwenye kuchukua hatua za kishujaa, lakini pia ujasiri ni kuwa tayari kutokuchukua hatua fulani ambayo ingekuwa kikwazo kwetu. Mfano mtu amekuudhi na hasira zikakujia, lakini ukajizuia usichukue hatua yoyote ukiwa na hasira hizi, hilo pia ni ujasiri.
Katika Kujijengea ujasiri zipo hatua tatu za kuchukua.
MOJA;HESHIMU MAPAMBANO.
Ni nzuri zaidi ukitambua kwamba safari ya mafanikio ni mapambano, ujue kwamba utakutana na magumu na changamoto. Hivyo usikimbie wala kutafuta njia rahisi badala yake, heshimu mapambano na uyapokee vizuri.
Kufikia mafanikio makubwa inahitaji kuweka kazi sana, kuwa na nidhamu ya hali ya juu, kujifunza kila wakati na kupambana na vikwazo vinvyoibuka kila wakati. Yote hayo yanahitaji ujasiri.
Tunaishi kwenye jamii ambayo inayaremba inawadanganya watu kwamba Kuna njia za mkato za kufanikiwa bila ya kuumia na bila ya kazi. Huo ni uongo na usijisumbue nao.
Uwe tayari kuumia, kuteseka na kuwa jasiri kupambana na hayo yote na mwisho wa siku utafanikiwa sana.
Mbili ;washirikishe wengine malengo yako makubwa.
Malengo makubwa uliyonayo kwenye maisha yeko, usiyafanye kuwa siri. Uwaeleze watu wazi kuhusu malengo haya.
Kwa kufanya hivi wataibuka watu wa kukupinga na kukushangaa. Wapo watakaokuambia umechanganyikiwa, wapo watakaokuambia hauwezi kabisa kufikia malengo haya makubwa. Lakini usiwasikilize hao, badala yake endelea kusimamia malengo yako.
Paza sauti kuelekea malengo yako makubwa ya maisha yako na unayofanyia kazi. Wengi watakupinga na kukucheka, lakini wapo watakaoweza kukusaidia na kuja kwako kuhakikisha unafikia malengo hayo.
Unahitaji ujasiri wa hali ya juu kuweza kuyaweka wazi malengo yako makubwa, kwa kufanya hivyo kunakuongezea ujasiri zaidi.
Pale mambo yanapokuwa magumu kwenye safari yako, ndiyo wakati wa kuuishi misingi yako kwa sababu hapo ndipo unapikwa kwa ajili ya mafanikio yako makubwa.
TATU ;TAFUTA MTU WA KUMPIGANIA.
Unapopewa jukumu la kumlinda mtu mwingine, unajitoa zaidi kujilinda mwenyewe. Mtu mwingine anapokuwa hatarini na wewe ni jukumu lako kumuokoa unapata ujasiri wa kuchukua hatua ambazo wewe mwenyewe usingeweza kuzichukua.
Angalia ni watu wa aina gani uko tayari Kuwapigania, upo tayari kufa kwa ajili yao. Watu hao watakupa wewe ujasiri wa kuwapigania hatua ambazo wewe mwenyewe usingeweza kuzichukua.
Kumbuka unafanya zaidi pale wengine wanapohusika kuliko unapokuwa mwenyewe.
Rafiki, hizi ndizo tabia tunazopaswa kuzijengea ili tuweze kufanikiwa zaidi. Tabia hizo kila mtu anaweza kujijengea bila ya kujali elimu, haiba, rangi, kabila au uwezo. Kazi ipo kwako na kwangu kuzijenga tabia hizo kwa kuchukua hatua tulizojifunza na maisha yetu yataweza kuwa bora.
Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio, ushauri nasaha na uandishi.
Maureen Kemei
Blog kufikirichanya.wordpress.com